Mnyeti auliza swali akidai halijajibiwa kwa miaka 20

Mnyeti auliza swali akidai halijajibiwa kwa miaka 20

Muktasari:

  • Mbunge wa Misungwi Alexander Mnyeti amekataa majibu ya Serikali kwamba hayana uhalisia kwa miaka 20.

Dodoma. Mbunge wa Misungwi Alexander Mnyeti amekataa majibu ya Serikali kwamba hayajabadilika kwa miaka 20 lakini hakuna utekelezaji wowote.

Mnyeti amesema majibu ya swali lake alipouliza kwa Wizara ya Maji yaliulizwa na wabunge wawili wawili waliomtangulia kwa nyakati tofauti tangu 2001.

Hata hivyo Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema anazo kumbukumbu kuwa wabunge wa Misungwi wa zamani walishawahi kuuliza na kujibiwa swali hilo.

Katika swali lake Mnyeti aliuliza Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji kwenye mji wa Usagara.

Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi amesema, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wilaya ya Misungwi ni asilimia 73.

Naibu Waziri amesema katika juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo, katika mwaka 2021/22 Serikali kupitia

Programu ya “Lake Victoria Water and Sanitation (LVWATSAN Program)” imepanga kutekeleza mradi wa maji katika maeneo ya Usagara, Buswelu, Kisesa na Buhongwa.

Amesema mradi huu utahusisha ujenzi wa vituo vya kusukuma maji mbili (2), mifumo ya usafirishaji na usambazaji maji yatakayozalishwa na chanzo kipya cha maji Butimba, ulazaji wa mabomba makubwa yenye ukubwa wa kuanzia milimita 50 hadi 600 kwa umbali wa  kilomita 50, ujenzi wa matanki manne (4) ya ukubwa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, utekelezaji wa mradi huo utanufaisha maeneo yote ya mji wa Usagara ikiwemo Usagara, Fela, Nyang’homango, Idetemya, Ukiliguru, Ntende, Sanjo, Isamilo, Mayolwa, Bukumbi na Kigongo.