MO Dewji azidi kutamba Afrika 

Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji 'MO Dewji'.

Muktasari:

  • Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Forbes jana Januari 30, 2023, Mo Dewji alikuwa nafasi ya 15 hapo awali, amepanda kwa nafasi mbili kutokana na utajiri wake unaokadiriwa kufikia Dola 1.5 bilioni (Sh 3.5 trilioni).

Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji 'MO Dewji amepanda kwa nafasi mbili katika orodha ya watu matajiri zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes akishika nafasi ya 13 kwa sasa huku akiongoza chati hiyo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika ripoti ya utafiti iliyotolewa na Forbes jana, Mo Dewji alikuwa nafasi ya 15 hapo awali, amepanda kwa nafasi mbili kutokana na utajiri wake unaokadiriwa kufikia Dola 1.5 bilioni (Sh 3.5 trilioni).
Mo ambaye anamiliki kampuni mbalimbali za vyakula, vinywaji baridi pamoja na kilimo amekuwa kichocheo kikubwa kwenye ukuaji wa uchumi na kukuza ajira nchini hasa kwa vijana.
Akizungumza baada ya kutajwa kwenye orodha hiyo, Mo amesema mkakati wake ni kuendelea kuongeza ajira kupitia kampuni zake ambapo, kwa sasa ameongeza ajira kutoka 28,000 hadi 35,000.
Hata hivyo, amesema kuwa mkakati wake ni kuzalisha ajira 100,000 ifikapo mwaka 2029.
“Tunashukuru mazingira ya biashara ni mazuri sana kwa sasa, azma yangu ni kuendelea kuongeza uwekezaji na kusaidia jitihada za Serikali kuzalisha ajira za kutosha,” alisema Mo Dewni.
Bilionea wa Nigeria aliyefanya uwekezaji wa uzalishaji saluji hapa nchini, Aliko Dangote anaongoza orodha hiyo ya watu matajiri zaidi Afrika akiwa na utajiri wa Dola 13.5 bilioni akifuatiwa na Johann Rupertwa Afrika Kusini mwenye utajiri wa Dola 10.7 bilioni.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), Dk Patrice Motsepe ambaye anamiliki klabu ya soka ya Mamelodi Sundowns, anashika nafasi ya tisa katika orodha hiyo akiwa na utajiri wa Dola 3.2 bilioni.
Ni orodha ambayo 10 bora yake imetwaliwa zaidi na mabilionea kutoka nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Misri mtawalia.
Nafasi ya tatu katika orodha hiyo inashikiliwa na  Nicky Oppenheimer(Afrika Kusini), nafasi ya nne yupo Abdulsamad Rabiu (Nigeria), nafasi ya tano kuna Nassef Sawiris (Afrika Kusini), akifuatiwa na Mike Adenuga (Nigeria), Issad Rebrab (Algeria), Naguib Sawiris (Misri), Motsepe (Afrika Kusini) na Mohamed Mansourwa misri.