MOI yaadhimisha miaka 26 ya huduma

Muktasari:

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ameongoza dua maalum ya maadhimisho ya miaka 26 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).


Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir ameongoza dua maalum ya maadhimisho ya miaka 26 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Dua hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za tiba pamoja na viongozi wa dini ambao kwa pamoja wameitaka taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma kwa upendo, ustahimilivu na kufuata maadili ya utumishi wa umma.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 5, 2022 Mufti, Sheikh Abubakar Zubeir amesema huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na taasisi hiyo zimewanufaisha wengi hivyo utendaji kazi ni wa wataalamu wa afya ambao ni mkono wa Mungu.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuachilia mkono wa baraka kwa watoa huduma madaktari, manesi, wahudumu na wote wanaohusika na kuwahudumia wagonjwa hawa kwa namna moja au nyingine,” amesema Mufti.

Naye, Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Denis Bwigira amesema katika utoaji wa tiba imani ni kuwa Mungu ndiye anayetenda hivyo akawatakia afya njema wahudumu wote ili watoe huduma kwa wagonjwa wanapofika kwenye taasisi hiyo.

“Mungu ijalie mafanikio zaidi kwa vifaa tiba, wataalamu na roho mtakatifu aweze kufanya kazi ndani ya wataalamu na kuzidisha imani kwa wale wanaowahudumia wajalie moyo wa uvumilivu, matumaini wale wanaokuja katika hali mbaya ya kiafya,” amesema Padri Denis.

Kiongozi wa Madhehebu ya Shia Tanzania, Azim Dewji amesema wahudumu katika taasisi hiyo wamekuwa wakifanya kazi zaidi ya masaa husika kwani wanafanya kwa moyo na si kwa muda wa ziada ili walipwe.

“Mikono yenu ni mikono ya Mungu. Madaktari wengi wa Muhimbili huwa hawaangalii pesa bali kutoa huduma,” amesema huku akitoa mfano wa Daktari bingwa wa upasuaji magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Hamis Shaban ambaye amekuwa akifanya vizuri na kukataa mialiko mingi ya kufanya kazi nje ya nchi.

Taasisi ya Mifupa MOI ilianzishwa mwaka 1996.