Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morogoro wajipanga kuongeza uzalishaji wa maziwa

Muktasari:

  • Mkoa wa Morogoro umeweka lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa hadi kufikia lita 50,000 kwa siku ndani ya miaka miwili, licha ya kukosa takwimu sahihi za sasa. Mkuu wa Mkoa, Adam Malima amesema wataelimisha wafugaji kuboresha mifugo yao na kutumia teknolojia bora.

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema licha ya mkoa huo kukosa takwimu sahihi za uzalishaji wa maziwa, wamejiwekea mikakati ya kuongeza uzalishaji hadi kufikia lita 50,000 ndani ya miaka miwili ijayo.

Malima amesema hayo leo Ijumaa, Mei 23, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya 28 ya kitaifa ya Wiki ya Maziwa, ambayo kitaifa yataadhimishwa Morogoro kuanzia Mei 27 hadi Juni mosi, 2025, katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro.

Amesema ili kuongeza uzalishaji wa maziwa, mkoa, kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa nchini, umepanga kutoa elimu kwa wafugaji hasa wa asili kuboresha mifugo, kwani ng’ombe wengi waliopo Morogoro wanazalisha maziwa chini ya lita moja.

“Katika maadhimisho haya ya wiki ya maziwa tutatoa elimu kwa makundi ya wafugaji, na kubwa tutazungumzia ufugaji wa kibiashara ili waongeze kipato, pia tukiwafundisha teknolojia bora za uzalishaji wa maziwa,” amesema Malima.

Amesema maziwa mengi yanayozalishwa Morogoro yanapotea wakati wa ukamuaji na usafirishaji, huku mengine yakikosa ubora kutokana na wafugaji wenyewe kutia maji.

“Afrika tunazalisha asilimia tatu tu ya maziwa yote duniani, hivyo kuna fursa kubwa kwa wafugaji wa Tanzania.

 “Hapa Morogoro tuna kiwanda cha kusindika maziwa ambacho kinahitaji lita 8,000 kila siku, lakini maziwa yanayotoka hapa hayafiki lita 2,000, mengine yote yanatoka mikoa mingine,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Bodi ya Maziwa nchini, Said Isike, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza chachu kwa wafugaji kufuga kitaalamu na kuongeza uzalishaji, kuifanya jamii itambue umuhimu wa kunywa maziwa, na kutoa fursa kwa wafugaji kutambua masoko ya mazao ya maziwa.

Amesema nchi ya Tanzania iko kwenye ukanda wa kitropiki, hivyo ufugaji wa ng’ombe wa mbegu kubwa ya kisasa ni mgumu, isipokuwa zipo koo maalumu za uzalishaji wa maziwa katika ukanda huo.

Ameshauri ng’ombe bora wa kufuga katika ukanda huo ni machotara, ambao wana uwezo wa kutoa lita 12 hadi 15 kwa siku, ambapo aina hiyo katika mikoa ya Njombe na Iringa wana uwezo wa kuzalisha maziwa lita 20 hadi 25.

Amesema, pamoja na kuwa kiburudisho, maziwa yana faida nyingi, ikiwemo kuimarisha mifupa, meno, na ni kinga ya mwili.

Kwa upande wake, mdau wa maziwa, Mshudwa Wilson, amesema kuna haja kwa bodi hiyo kudhibiti uuzaji holela wa maziwa yanayowekwa kwenye chupa za plastiki, kwani ni hatari kwa afya za watumiaji kutokana na uandaaji wa maziwa hayo.

“Sasa hivi ukizunguka kwenye maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro, utakuta watu wanauza maziwa kwenye chupa za maji. Tunashindwa kujua usafi wa zile chupa, utayarishaji wa yale maziwa kuanzia kwenye ukamuaji mpaka kwenye kupakia. Ni vyema bodi ikatazama upya hili,” amesema Isike.a