Morogoro yaongezewa Sh2 bilioni bajeti ya miundombinu

Muktasari:

Serikali imeongeza bajeti ya fedha kwa mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matengenezo ya barabara na miundombinu mingine kutoka Sh24.8 bilioni kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh26.02 bilioni mwaka 2021/2022.

Morogoro. Serikali imeongeza bajeti ya fedha kwa mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matengenezo ya barabara na miundombinu mingine kutoka Sh24.8 bilioni kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh26.02 bilioni mwaka 2021/2022.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella alisema hayo wakati akifungua kikao cha 37 cha bodi ya barabara ya mkoa huo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Shigella alisema licha ya Serikali kuongeza bajeti hiyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wabunge wa mkoa huo kusaidia upatikanaji wa fedha za kutosha za maendeleo kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu hususani ya barabara.

“Katika kikao hiki niwaombe waheshimiwa wabunge wetu wa mkoa wa Morogoro kupaza sauti bungeni ili zipatikane fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ikiwemo ya Bigwa-Kisaki inayoelekea Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere  na kwenye bwawa la kuzalisha umeme wa megawati 2,115,“alisema Shigella.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ongezeko hilo ni pamoja na  upande wa bajeti ya maendeleo kutoka Sh2.75 bilioni ya mwaka wa fedha 2020/2021 na kufikia Sh5.37 bilioni mwaka 2021/2022.

Shigella ameongeza kuwa Serikali imetoa Sh2.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bigwa-Kiroka kwa urefu wa kilometa 15 katika kiwango cha lami.

Kwa upande wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), alisema bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa ni Sh400 milioni na bajeti ya mwaka 2021/2022 imeongezeka hadi kufikia Sh23.93 bilioni.

Shigella alisema kwa upande wa matengenezo ya barabara katika mwaka wa fedha 2020/2021 ilitengewa Sh8.07 bilioni na mwaka huu wa 2021/2022 imeongezeka kufikia Sh8.23 bilioni.

Wakijadili kwa nyakati tofauti akiwemo Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo waliipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti katika sekta ya miundombinu ya Barabara.

Mbali na hayo wengine walipongeza utendaji mzuri wa kazi wa Tanroads na Tarura huku wakiwataka watendaji hao kuongeza juhudi kiutendaji badala ya kubweteka na pongezi zilizotolewa kwao.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Mhandisi  Baraka  Mwambage alisema licha ya  mafanikio yaliyopatikana bado kunachangamoto  ya ufinyu wa bajeti  kulingana na mahitaji halisi .

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro pia alitaja kuwepo kwa uvamizi wa hifadhi ya barabara, wizi, uharibifu alama za barabarani pamoja na uzidishaji wa uzito kwenye mizani.

Mbali na changamoto hizo alisema hatua na mikakati mbalimbali imechukuliwa ikiwa na kutolewa kwa elimu kwa wasafirishaji sambamba na kuwaelimisha kuhusu sheria ya udhibiti uzito ya Afrika Mashariki.