Morris: Nawaachia vijana Stars

New Content Item (1)
Morris: Nawaachia vijana Stars

Muktasari:

Beki mkongwe wa timu ya Taifa ‘Taif Stars’, Aggrey Morris, jana alistaafu rasmi kuichezea timu hiyo, akiwa amefanya hivyo pia katika timu ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ baada ya kulitumikia taifa kupitia mchezo wa soka kwa zaidi ya 15.

Zanzibar. Beki mkongwe wa timu ya Taifa ‘Taif Stars’, Aggrey Morris, jana alistaafu rasmi kuichezea timu hiyo, akiwa amefanya hivyo pia katika timu ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ baada ya kulitumikia taifa kupitia mchezo wa soka kwa zaidi ya 15.

Morris anaondoka katika timu mbili za taifa akiwa ameichezea Stars kwa miaka 11 huku ile ya Zanzibar akiitumikia kwa miaka 16.

Beki huyo wa kati anayeichezea Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara Azam alianza kuichezea Stars 2009, huku Zanzibar Heroes alianza kuitumikia 2004.

New Content Item (1)
Morris: Nawaachia vijana Stars

Baada ya kutangaza kustaafu wiki iliyopita, jana Stars ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam pia ilikuwa maalumu kwa ajili ya kumuaga nahodha huyo wa Azam.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi mjini hapa, ambako timu yake ya Azam ilikuwa inashiriki michuano ya Mapinduzi, Morris alieleza mambo mbalimbali yanayohusiana na maisha yake ya soka, milima na mabonde pamoja na mafanikio aliyopata.

“Ni wakati wa kuachia kijiti kwa wengine kama nilivyoachiwa mimi, umri umeenda na nimecheza kwa muda mrefu, naamini mchango wangu nilioutoa ni mkubwa pia. Ni wakati wa vijana nao kuonyesha kile walichonacho sasa maana wapo wengi wazuri wanaocheza nafasi kama yangu,” anasema Morris ambaye umri wake ni miaka 36.

“Sijastaafu Stars pekee, bali hata Zanzibar Heroes ambapo mara ya mwisho niliitwa kikosini, lakini nilimweleza kocha kuwa sasa ni wakati wa kustaafu ili wengine wacheze maana hata Zanzibar kuna vijana wengi wazuri wenye uwezo wa kucheza kwa mafanikio makubwa, kocha All Bushiri alinielewa hilo.”

Kama ilivyo kwa wansoka wengi, Morris pia alianza kutengeneza jina akichezea timu ndogondogo.

“Nilianza kucheza timu za madaraja ya chini hapa Zanzibar na baadaye nilijiunga na timu ya Mafunzo FC chini ya kocha Mshenga (marehemu), huyu ndiye aliyeniona hasa kwamba nina kitu cha kufanya kwenye mpira.”

“Kocha huyo nakumbuka alituchagua wacheza saba ambapo nilicheza kwa miaka mitano na kujiunga Azam FC. Nikiwa Mafunzo nilibahatika kuichezea kombaini ya Zanzibar ambayo ilishiriki mashindano ya Karume Cup.

“Mashindano hayo sidhani kama yapo mpaka sasa hivi, ingawa wakati wetu tulichukua ubingwa, baadaye pia nilichaguliwa kuichezea Zanzibar Heroes ambayo nimeichezea kwa miaka 10,” anasema ambaye alijiunga na Azam kwenye dirisha la usajili la 2009.


Azam FC

Anasema ana mkataba wa mwaka mmoja na miezi minane na Azam FC, hivyo ukimalizika nako atastaafu rasmi na kufanya shughuli zingine ingawa alianza kusomea mambo ya ukocha.

“Hata huku mkataba wangu ukimalizika nastaafu na kufanya mambo mengine, naamini Azam ina wachezaji wengi wazuri wanaoweza kucheza kwenye ubora mkubwa kama mimi ama zaidi,” anasema Morris ingawa hakutaka kuweka wazi nini atafanya baada ya kustaafu soka.”

Hata hivyo, habari ambazo Mwananchi limezipata kutoka ndani ya Azam ni kwamba mchezaji huyo akistaafu atapatiwa kazi katika benchi la timu hiyo.

Pacha bora

Kuhusu wachezaji anaowahusudu katika maisha yake ya soka, Morris anawataja Kevin Yondani na Nadir Haroub ‘Canavaro’ kuwa ndio walikuwa pacha bora akiwa Stars.

Wachezaji hao wawili waliichezea Yanga ambapo Canavaro alistaafu soka na ni neneja wa Stars kwa sasa wakati Yondani yupo Polisi Tanzania.

“Nilikuwa nafurahi zaidi nikicheza na mmoja wapo kati ya Yondani au Canavaro, nilicheza kwa kuufurahia zaidi mpira, kiukweli hizo ndizo pacha zangu bora za wakati wote.” anasema.

Namba Azam, Stars

Morris anasema alipotua Azam na Stars kote alikutana na ushindani wa namba kwani aliwakuta wachezaji waliokuwa kwenye viwango vya juu zaidi.

“Azam walikuwepo kina Said Swedy ‘Kussy’, Said Morad, Atudo kutoka Kenya, David Mwantika, Canavaro na sasa wapo kama Yakubu Mohamed, Daniel Amour, Abdallah Kheri na Oscar Masai.

“Stars nilikutana nao kama Kussy, Canavaro, David Naftali, Juma Nyosso na wengine ambao kiukweli walikuwa vizuri, lakini ili ufanikiwe ni lazima uzingatie mafunzo ya kocha pamoja na kujiongeza binafsi,” anasema.

“Kikubwa ambacho nilikuwa nakipenda Stars ni wakati ule wa kocha Mbrazil Marcio Maximo alipenda kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya kurithi nafasi za watu kwa baadaye na hivyo ndivyo inavyotakiwa, mchezaji anapaswa kuandaliwa kwa malengo ya baadaye na sio kubadilisha badilisha tu wachezaji, mpira unaandaliwa ili uwe katika ngazi nzuri.

“Niliowakuta walipewa nafasi wakati wengine tukiendelea kujifunza hivyo tulivyoanza kucheza tayari tulikuwa tumeandaliwa maana tulijifunza pia kwa waliotutangulia, ndiyo wachezaji walikuwa imara zaidi.”

Kocha bora

Akizungumzia makocha waliomfundisha, anasema amepitia kwa wengi, lakini Stewart Hall ndiye bora kwake kwa nyakati zote.

“Hall alivyokuja alikuta wachezaji hatujui lolote kuhusu mpira ingawa tunacheza, alitufundisha zaidi ya ukocha wake tukaujua mpira na tukaufurahia, yaani Azam alianza nayo kama akademi tu hivyo tulielewa mambo mengi,” anasema.

“Huyo kwangu atabaki kuwa kocha bora wa nyakati zote, anajua mpira na anajua kuufundisha na namna gani mchezaji anatakiwa kuwa, wakati wa mazoezi na wakati wa mechi, mafunzo yake tuliyajua vyema na kuyafanyia kazi kwa mafanikio makubwa.”


Kuyumba kwa Azam FC

Azam FC ni timu iliyowekeza kwa kiasi kikubwa, lakini haina mafanikio makubwa hasa kwenye Ligi Kuu Bara ukiachana na ubingwa iliowahi kuchukua kwenye mashindano ya Kagame na Kombe la Mapinduzi.

“Ni kweli Azam kwa sasa haina matokeo mazuri, lakini katika soka ni kitu ambacho kipo, hata ukiangalia timu za Ulaya zina uwezo mkubwa kipesa na zimewekeza, lakini ukija kwenye ligi matokeo si mazuri, naamini Azam itakaa sawa na kupata kile kilichowekwa kwenye malengo,” anasema

“Ligi Kuu tumetwaa ubingwa mara moja, lakini mashindano mengine tumetwaa mara nyingi hayo - pia ni mafanikio, malengo ya Azam ni kutwaa ubingwa wa ligi hivyo yapo na yanaendelea kupambaniwa ila tu hatujayafikia kama ilivyokusudiwa.”


Mafanikio na Changamoto

Morris anasema kupitia soka amepata mafanikio mengi ingawa hapendi kuyaanika akisisitiza kuwa: “Mpira umenipa mafanikio mengi na hii yote ni kwa sababu nimeuheshimu na umeniheshimu, na ndio maana pia nimecheza kwa muda mrefu, najivunia hilo.”

Kuhusu changamoto, mchezaji huyo mkongwe anasema zipo kadhaa, lakini moja iliyomuweka katika wakati mgumu ni pale alipotuhumiwa kuihujumu Azam FC.

“Usipokuwa na moyo wa ujasiri unaweza kukata tamaa kucheza mpira, lakini changamoto ni nyingi sana ambazo kama mchezaji ili uwe bora ni lazima ukabiliane nazo “Binafsi nimekutana nazo nyingi hata kabla sijaingia Azam, nikiwa timu ya Karume niliwahi kuvuliwa jezi nikiwa benchi na kuvalishwa nguo nyingine, iliniuma sana.”