Moshingi Bosi mpya DCB
Muktasari:
- Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara ya DCB, imemtangaza Sabasaba Moshingi kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo kufuatia nafasi hiyo kukaa wazi kwa mwaka mzima.
Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya DCB, imemtambulisha Sabasaba Moshingi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake mpya, akijaza nafasi inayoelezwa kuwa wazi kwa “muda mrefu” tangu kuondoka kwa aliyekuwa katika nafasi hiyo.
Moshingi anachukua nafasi hiyo akitokea benki ya TCB ambako alikuwa Mkurugenzi Mtendaji, huku akiwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika benki za Standard Chartered, Stanbic na KCB.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo jijini hapa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Zawadia Nanyaro amesema iliwachukua muda mrefu kutafuta mtu sahihi wa kuchukua nafasi hiyo.
"Ni matumaini yetu, wateja wetu na wanahisa wetu kwamba ujio wa Moshingi umekuja kwa wakati sahihi na kutokana na historia ya mafanikio aliyoyapata katika taasisi alizowahi kufanya kazi, tunaiona benki yetu ikizidi kupanda kuelekea mafanikio,” amesema na kuongeza;
"Moshingi ni mtaalamu mzoefu wa masuala ya benki kwa zaidi ya miaka 21, ambaye anakuja kwetu akiwa na hazina kubwa ya uzoefu katika tasnia za kibenki za kitaifa na kimataifa. Ana rekodi thabiti katika uendeshaji wa benki, biashara, huduma kwa wateja, masuala ya mikopo na mengineyo."
Moshingi ana shahada ya uzamili ya utawala wa biashara katika fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) na amethibitishwa na Taasisi ya Mabenki Tanzania.
Akizungumzia maendeleo ya benki hiyo, Nanyaro amesema DCB inazidi kupiga hatua huku ikiendelea na jukumu mama la kuanzishwa kwake tokea miaka 21 iliyopita.
“Jukumu hilo ni kutoa huduma bora za kifedha ikijikita zaidi katika kusaidia miradi endelevu ya kupunguza umasikini na kuendeleza jamii kwa kutoa huduma na bidhaa zenye ubunifu kwa wateja,” amesema.
Kwa upande wake Moshingi ameishukuru bodi hiyo na wanahisa wake kwa kuwa na imani naye akiahidi kutumia uzoefu wake alioupata katika kutumikia taasisi mbalimbali za fedha kuipa mafanikio benki hiyo.
"Nikiwa na uzoefu wa miaka mingi katika maeneo ya biashara za kifedha, mikopo na wateja binafsi, ni matumaini yangu kuwa kwa pamoja tutaendeleleza azma hii kwa kutoa suluhu nyingi zaidi za mitaji kwa wafanyabiashara wadogo,” amesema Sabasaba Moshingi.
Ameongeza kuwa “Huduma hizo tutazitoa kwa wakati, lakini pia tutaangalia kwa masuala yahusuyo uboreshaji wa huduma za kifedha kwa njia za kidigitali ili zilingane na mahitaji ya Watanzania.”
Moshingi anachukua nafasi hiyo ambayo imebaki wazi kwa takribani mwaka mmoja tangu kuondoka kwa Godfrey Ndalahwa aliyekuwa katika nafasi hiyo.