Moto mlima Kilimanjaro waendelea kudhibitiwa kilometa za mraba 2.5 zikiteketea
Muktasari:
Moto uliowaka katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro kwa siku tatu mfululizo unaendelea kuzimwa na eneo kubwa likidhibitiwa huku eneo la kilometa za mraba 2.5 kati ya kilomita za mraba 1,712 zikiwa zimeathiriwa na moto huo.
Moshi. Moto uliowaka katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro kwa siku tatu mfululizo unaendelea kuzimwa na eneo kubwa likidhibitiwa huku eneo la kilometa za mraba 2.5 kati ya kilomita za mraba 1,712 zikiwa zimeathiriwa na moto huo.
Moto huo ambao bado chanzo chake hakijajulikana ulianza Oktoba 21 mwaka huu katika eneo la Karanga kuelekeaBaranco mita 3,963 kutoka usawa wa bahari ambapo mpaka sasa hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza.
Tayari wadau zaidi ya 500 wakiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, Jeshi la akiba, askari wa Tanapa, wanafunzi kutoka chuo cha usimamizi wa wanyamapori (Mweka) na wadau wengine wapo katika eneo hilo kuudhibiti moto huo usisambae kwenye maeneo mengine.
Akizungumza na waandishi leo Jumapili Oktoba 23, 2022 katika lango la Mweka, Waziri wa Maliasili na utalii, Dk Pindi Chana amesema juhudi za kuzima moto huo zinaendelea na tayari vikosi vinavyoendelea na kazi ya kuzima moto vimefanikiwa kuudhibiti moto huo katika maeneo mengi ya mlima huo.
"Moto uliokuwa unawaka kutoka katika kituo cha Millenium kuelekea Marangu Hut na Mweka Hut nao umedhibitiwa kabla ya kufika katika vituo hivyo, juhudi zaidi zimeelekezwa eneo lenye korongo kubwa la Karanga ambapo vikosi vinavyoendelea na kazi ya kuzima moto viko katika eneo hilo kuhakikisha moto huo pia unadhibitiwa" amesema Dk Chana
"Mpaka sasa zoezi linaendelea vizuri na tuna matumaini makubwa ya kudhibiti moto huu kadri muda unavyokwenda. Navishukuru yombo vya ulinzi na usalama, taasisi mbalimbali za Wizara ya Maliasili na Utalii, wadau wa utalii na uhifadhi kutoka makampuni mbalimbali ya Utalii hapa nchini, wanahabari mashirika na wananchi kufuatia juhudi walizoonyesha kuhakikisha mlima wetu unakuwa salama," amesema
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo amewaagiza wataalamu kufanya tathmini na utafiti ili kuweza kubaini chanzo cha moto katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro ili kudhibiti kujirudia mara kwa mara.
"Nimefika eneo la tukio nimeona kazi ya kuudhibiti moto inakwenda vizuri na mafanikio ni makubwa, ila tumewaelekeza wataalamu, mara baada ya kuudhibiti moto huu, sasa ifanyike tathmini na utafiti kubaini nini kilitokea"
"Hatuwezi kujua nini kilisababisha moto huu, hivyo ifanyike tathmini na utafiti kubaini chanzo cha moto ili kudhibiti hali hii kujirudia mara kwa mara na kuepusha athari zinazoweza kutokea za kimazingira lakini pia za maliasili na utalii" amesema
"Niwatoe hofu watanzania, hali ni nzuri na nimefika eneo la tukio, watalii wanaendelea na shughuli za utalii bila shida yoyote na zaidi ya timu ya watu 459 wapo wakiendelea kuudhibiti moto huo"
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), William Mwakilema amesema hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 1,712 na eneo lililoathiriwa na moto huo ni kilometa za mraba 2.5 sawa na asilimia 0.4.
"Tumefuatilia kwa picha za setilite jana usiku moto ulikuwa kwenye eneo moja na leo asubuhi moto ulikuwa umepungua sana na saa 11 jioni ya leo tumefuatilia picha inaonyesha moto umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kwa sasa nguvu itaendelea kuwepo na vikosi vilivyopo vitapitia maeneo yote kuhakikisha moto umeisha,"
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo na kudhibiti matukio hayo kujirudia.