Mpango amesema alipoachiwa nchi aliogopa

Saturday September 25 2021
mpangopicc

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, amesema aliogopa alipoachiwa nchi wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliposafiri kwenda nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa ambao uliwashirikisha viongozi wa mataifa mbalimbali.

Mpango alitoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 25, 2025, katika hafla ya kumpokea Rais Samia, iliyofanyika uwanja wa ndege wa Terminal 1.

Amesema katika kipindi ambacho Rais Samia akiwa safari alikuwa anaogopa na kujiuliza likitokea jambo la kumtisha atafanyaje lakini anashukuru amesimamia vema na mpaka Rais anarudi ameikuta nchi salama.

“Kipindi chote ambacho Rais hakuwepo nilikuwa naogopa nasema sasa likitokea jambo la kunitisha nafanyaje, lakini Rais nchi yako ipo salama salmini,” amesema Dk Mpango.

Amewashukuru Watanzania kwa kudumisha utulivu na amani.

“Napenda nikuhakikishie kuwa nchi yako ipo shwari, ipo salama imetuulia kama maji kwenye mtungi, kipindi chote ambacho hukuwepo wananchi wamekuwa watulivu na wana kila sababu ya kusheherekea kukupokea,” amesema Mpango.

Advertisement

Pia amempongeza Rais Samia kwa namna alivyoibeba Tanzania kwa kusoma hotuba nzuri katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kwa kutulia.

“Tumefuatilia hotuba yako na ziara yako kule Marekani, sisi ambao tuliwahi kuwa kwenye kile chumba cha mkutano kiukweli umetubeba, Mungu aendelee kukutunza,” amesema Mpango.

Advertisement