Mpango usafirishaji wa dharura wazazi, watoto wachanga wazinduliwa Arusha
Arusha. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamezindua mpango wa usafirishaji wa dharura za wazazi na watoto wachanga mkoa wa Arusha ujulikanao kama m-mama ambao utawezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma ya mama na mtoto kutoka kituo kimoja kwenda kingine kwa wakati.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mt Meru, Mkuu wa kanda ya kaskazini Vodacom, George Venanty amesema kuwa mpango huo utasaidia sana kuokoa vifo vitokanavyo na mama na mtoto.
Amesema kuwa, Vodacom wamekuwa washiriki katika mradi huo katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mafanikio na kuweza kupunguza vifo vya wakinamama .
Aidha Venanty amesema uwepo wa mfumo huo unaweza kuondoa changamoto ya ufinyu wa magari ya wagonjwa (ambulance) uliopo kwani watakuwa wanatumia magari ambayo yapo kwenye mfumo kwa muda wowote ambayo tayari yalishaandaliwa kwa kazi hiyo.
"Wahudumu wa afya watumie mfumo huo kuhakikisha wanaokoa vifo vya wanawake na watoto wachanga hivyo naomba sana mchukulie kwa uzito ili uweze kufanikiwa kwani mfumo huu tayari tumeuzindua katika mkoa wa Manyara na hadi kufikia Septemba mwaka huu tutakuwa umefika mikoa yote," amesema Venanty
Muuguzi Mkuu wa mkoa na Mratibu wa mpango wa m-mama kwa mkoa wa Arusha, Getrude Anderson amesema ni mpango wa usafirishaji kwa wakina mama wajawazito ambao wanapata dharura na kuweza kuhamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.
"Endapo akitokea mgonjwa ambaye amepata dharura wakati wa kujifungua wanaangalia gari ambayo ipo karibu kwani tayari walishaingia mkataba na madereva mkoa mzima hivyo wanachofanya ni kuchagua gari na kufika kituo kilicho karibu na kuweza kutoa huduma ya haraka kwenda kituo kingine," amesema.
Amesema kuwa, uwepo wa huduma hiyo unarahisisha kwa kiwango kikubwa sana kwani badala ya gari kutembea umbali wa kilometa mia mbili inatembea umbali wa kilometa mia moja tu .
"Nawaomba sana watumishi tuutumie mfumo huu kwani utaweza kuokoa maisha ya mama na mtoto na kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za wakinamama "amesema Getrude.
Ofisa elimu wa mkoa wa Arusha, Abel Ntupwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, amesema mfumo huo utaleta suluhishi la changamoto ya upatikanaji wa usafiri wa dharura kwani ambulance za serikali zilizopo hazitoshi.
Aidha amesema mpango huo utaongeza hali ya furaha na kujiamini kwa wanawake na hivyo ni vizuri kila Mtanzania akafikiwa na huduma hiyo kwani ni ubunifu wa hali ya juu hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha anaunga mkono mpango huo.