Mpango wa Taifa na kuimarisha muungano

Thursday June 10 2021
kuimarishapic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Serikali imesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 utaendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk  Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema miradi itakayotekelezwa kwa pamoja Tanzania bara na Visiwani ni pamoja na kukarabati na kujenga ofisi na makazi ya makamu wa rais Wete - Pemba na Kilimani mjini Dodoma pamoja na kukamilisha ukarabati wa ofisi na makazi ya makamu wa rais Tunguu, Zanzibar.

“Pia kuongoa ardhi iliyoharibika na kuboresha kingo za mito katika maeneo ya Kaskazini A (Unguja) na Kishapu (Shinyanga) katika maeneo ya mradi kwa kutekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kupitia mifumo ya ikolojia.“

“…na mpango wa kunusuru kaya masikini Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) ambapo shughuli zilizopangwa ni kutambua na kutathmini hali za ustawi wa maisha ya kaya 886,724 za walengwa wa mpango na kuhawilisha ruzuku kwa kaya maskini 1,146,723 katika maeneo 186 ya utekelezaji kwa mizunguko sita ya malipo Tanzania bara na visiwani,” amesema.

Advertisement