Mradi wa kidijitali Africa Connect kuwanufaisha wakulima 133 Korogwe

Afisa Kilimo cha Umwagiliaji na Ushirika wilaya ya Korogwe, Ramadhan Sekija akimkabidhi mfuko wa mbolea mkulima wa mpunga skimu ya Mombo, Said Mohamed.

Muktasari:

  • Wakulima wanaolima mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Mombo wilayani Korogwe mkoani Tanga kunufaika na mradi mpya wa kidijitali.

Korogwe. Wakulima wanaolima mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Mombo wilayani Korogwe mkoani Tanga kunufaika na mradi mpya wa kidijitali.
Hayo yamebainishwa na Meneja mradi wa Africa Connect kutoka kampuni ya YARA, Deodath Mtei wakati wa ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima wa skimu ya umwagiliaji ya Mombo.
Amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza tija katika kilimo cha mpunga kwa kutoa mafunzo kwa wakulima.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali na kutoa mafunzo kwa wakulima hasa katika matumizi bora ya pembejeo za kilimo ili kwa pamoja tuweze kuendeleza kilimo cha mpunga” amesema Mtei.
Amesema huduma hiyo inalenga kuhakikisha wakulima wanafuata ubora katika hatua zote za kilimo ili waweze kuvuna mazao bora.
Aidha Mtei amebainisha kwamba wanaita kilimo cha kidijitali kwa sababu kimeunganishwa katika kifurushi cha wadau wa kilimo kutoka Equity Benki, wakala wa mbegu za kilimo ASA na wanunuzi wa mpunga Murzah Wilmar, na kwa kutumia mfumo huo mkulima anaweza kupata mkopo usiokuwa na dhamana ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Mpunga wilayani Korogwe, mzee Hamisi Saidi amesema mradi huo umewanufaisha kwa kuwa na uhakika wa kupata mavuno mengi ukilinganisha na hapo awali ambapo kwa sasa wanavuna maguni 40 kwa heka moja.
"Mradi huu unatunufaisha, kwanza tumepewa mabwana shamba ambao wanatupa elimu ya matumizi bora ya pembejeo lakini pia kututafutia masoko hivyo tunalima kilimo cha biashara ambapo tunapata chakula na pia tunauza kwa kuwa tuna uhakika wa soko" Amesema mzee Saidi.
Mradi huo ulizinduliwa Mei 20 mwaka huu jijini Dodoma ukiwa na lengo la kuwafikia wakulima laki moja katika mikoa 9 ya Tanzania Bara.