Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa maji Nasuro-Same wazinduliwa

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, Abdalla Shaibu akimtwisha ndoo ya maji, mmoja wa kina mama wa kijiji cha  Nasuro wilayani Same, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mradi wa Maji Kirinjiko.

Muktasari:

  • Mradi huo ambao umezinduliwa leo Juni 20, 2023 na Mwenge wa uhuru, umegharimu Sh662.1 milioni hadi kukamilika, ambapo umetajwa kuondoa adha kubwa ya maji ambayo wananchi walikuwa wakikabiliana nayo.

Same. Zaidi ya wananchi 2,643 wa kijiji cha Nasuro na maeneo jirani, wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, baada ya mradi wa maji wa Kirinjiko kukamilika.

Mradi huo ambao umezinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru wilayani hapa, umegharimu Sh662.1 milioni hadi kukamilika kwake ambapo umetajwa kuondoa adha kubwa ya maji ambayo wananchi walikuwa wakikabiliana nayo.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Same, Abdallah Ally amesema mradi huo ulianza kutekelezwa januari 24,2022 na kwa sasa uko kwenye muda wa matazamio hadi oktoba 15,2023.

Aidha amesema Wilaya ya Same imekuwa ikichukua hatua za makusudi ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi, ambapo kutokana na jitihada hizo upatikanaji wa huduma hiyo umeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 75.2 mwaka huu.

"Mradi huu wa maji wa Kirinjiko unatoa huduma kwa wananchi 2,643 wa Kijiji cha Nasuro,lakini Wilaya hii inaendelea kufanya jitihada ili kuongeza mtandao wa maji ndani ya Wilaya kwa kutekeleza miradi ya maji ya Mabilioni, Bombo, Sesemi -Bendera, Gwanga-Marieni na Vuje, mradi wa maji Ndungu, Kirangare pamoja na Mroyo-Kisangaze"

Akizungumza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim amesema mradi huo ni moja ya jitihada za kumtua mama ndoo kichwani na kuomba jitihada hizo ziendelee kuungwa mkono.

"Baada ya kupokea taarifa ya kina inayohusiana na mradi huu wa maji na kufanya ukaguzi, tuwapongeze viongozi kwa kazi kubwa ambayo mmefanya kwani mradi huu tunaamini unakwenda kumtua mama ndoa kichwani, lakini pia tunaamini upo uendelevu wa miradi ya maji, naomba tuunge mkono jitihada hizi," amesema.

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nasuro, wamesema upatikanaji wa maji katika kijiji hicho ni faraja kwa kuwa sasa wameondokana na adha ya kwenda kusaka huduma huyo katika vijiji vya mbali.

"Tumepata tabu sana ya maji, tumekuwa tukichota Mwembe na Punda, lakini kwa sasa tumesogezewa huduma hapa karibu, tuwashukuru wote walioona umuhimu huu, kwani tutaweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo" amesema Fatuma Mwarabu.

Katika Wilaya ya Same ambako mwenge umepokelewa ukitokea mkoani Tanga, umekimbizwa Kilometa 99.6 ambapo umetembelea miradi saba yenye thamani ya Sh3.6 bilioni.

Mbali na mradi wa maji, miradi mingine iliyotembelewa na Mwenge ni pamoja na ufunguzi wa barabara ya Hedaru -Vunta-Myamba, uzinduzi wa madarasa Mawili katika shule ya Sekondari Chauka, kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, kuweka jiwe la msingi Zahanati ya Saweni na kugawa vyandarua.