Mradi wa Sh7.5 bilioni kupinga ukatili wa kijinsia waja

Dar es Salaam. Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo la GIZ wamesaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wenye thamani ya Euro 3 milioni sawa Sh7.5 bilioni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo amesema mradi huo wa miaka mitatu utajikita katika kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto.

"Tunahitaji kuwajengea uwezo na kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo mbalimbali, hivyo huu utakuwa ni moja ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara," amesema Makondo wakati wa kusaini makubaliano hayo katika hafla iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa GIZ, Dk Mike Falke na Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess.

Makondo amesema kuna sheria na sera nzuri nchini, lakini bado wanawake wanahitaji kujengewa uwezo zaidi wa namna ya kupata haki zao na kupata msaada wa kisheria.

"Mradi huu utaunganishwa na kampeni ambayo Wizara inautekekeza ya huduma za msaada wa kisheria," amesema Makondo akiishukuru GIZ na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano.

Kwa upande wake, Dk Falke amesema ukatili wa kijinsia ni changamoto katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

"Tunaamini mradi huu utakwenda kuwa suluhuhisho katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini Tanzania," amesema.