Mshtakiwa kesi ya maiti iliyozikwa ‘mlangoni’ augua mahakamani

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

Mshtakiwa wa kesi ya mauaji ya mkatisha tiketi, mkazi wa Ilala, Jijini Dar es Salaam, ameugua mahakamani na kusababisha kesi yake kuahirishwa mpaka kesho.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu imelazimika kusimamisha usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mkatisha tikesi wa mabasi ya kampuni ya Waida, Farahan Abdusalum, baada ya mshtakiwa Hemed  Hamisi Ally  kuugua.

 Kesi hiyo inayosikilizwa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi, Joyce Minde, aliyepewa mamlaka ya ziada kusikiliza kesi hiyo ambayo kisheria ilipaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ilipangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka leo  Alhamisi, Septemba 22, 2022.

Upande wa mashtaka kupitia mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Aziza Mhina ameieleza mahakama walikuwa na mashahidi wawili, akiwemo mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kwamba walikuwa tayari kuendelea.

Hata hivyo, mshtakiwa alinyoosha mkono juu na wakili wake, Fredrick Charles alimfuata na kunong’ozenana naye kisha akaieleza mahakama mshtakiwa huyo amemueleza anajisikia vibaya kwa kuwa anasubumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa sukari.

Kutokana na taarifa hiyo, Hakimu Minde amesema  kutokana na hali hiyo haitawezekana kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo, hiyvo akaiahirisha mpaka kesho asubuhi saa 2:00 itakapondelea kama mshtakiwa atakuwa katika hali nzuri.

Ally anadaiwa kumuua Farahan, Juni 12, 2014 maeneo ya Sharifu Shamba Ilala, jijini Dar es Salaam kisha akauzika mwili wake nje karibu kabisa na mlango wa kuingilia katika nyumba aliyokuwa akiishi.

Hata hivyo, mwili huo ulifukuliwa na Jeshi la Polisi Februari 9, 2015, takribani miezi minane baadaye kwa ajili ya uchunguzi, baada ya polisi kupata taarifa kuwa mshtakiwa alimuua na kuuzika mwili huo na kisha mshtakiwa mwenyewe kuwaongza polisi mahali alipouzika.