Msiba wa ajuza wamwibua Spika Tulia Mbeya

Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini,Dk Tulia Ackson akisalia wananchi wa mtaa wa kabisa  mara baada ya kushiriki ibada ya kuaga mawili kikongwe, Angetile Kajumba (85) nyumba kwake. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo leo Jumapili June 4,2023 aliposhiriki ibada ya kuaga mwili wa kikongwe   Angetile Kajumba (85 ) aliyepoteza maisha kwa  kukosa huduma muhimu za  matibabu , baada ya kutelekezwa na  familia yake.

Mbeya. Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson amekemea tabia ya baadhi ya familia kutekeleza wazazi kwa kushindwa kuwahudumia na kuagiza uongozi wa serikali za mitaa kutoa taarifa za watu hao katika ngazi husika.

Dk Tulia ameyasema hayo leo June 4, 2023 mara baada ya kushiriki ibada ya kuaga mwili wa Angetile Kajumba (85) ambaye alifariki Mei 3, 2023 kutokana na kuugua kwa muda mfupi na kukosa huduma za afya .

“Nashangaa hapa Marehemu  alikuwa analelewa na wananchi na hata Taasisi yangu ya Tulia Trust ilipata taarifa akiwa hai na  kufika kukarabati nyumba aliyokuwa akiishi na kumnunulia mahitaji lakini leo nasikia kuna watoto wake wanalia kwa uchungu  siku zote walikuwa wapi?,”amehoji

Ameongeza kuwa“Wenyeviti wa Serikali za mitaa toeni taarifa za hawa watu wanao watelekeza wazazi kwa kweli hilo halipendezi kabisa sasa hapa ndugu wanalia nini? na hata rambirambi zikitolewa anakabidhiwa nani kama wananchi hatutambui kama ana familia msiba huu ni wetu,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisunga Kata ya Mabatini, Ajuaye Kyando amesema kitendo kilichofanywa na familia ya marehemu sio cha kiungwana kwani baada ya kupata ulemavu familia yake alitelekezwa na kulelewa na jamii.

“Marehemu ameishi maisha ya tabu sana na hata tulipokuwa tukishirikisha familia yake ilikuwa haitoi  ushirikiano mpaka umauti ulipomfika na kama mtaa tumepoteza mtu muhimu ambaye licha ya changamoto za ulemavu alikuwa mshauri ”amesema.

 Diwani wa Kata ya Mabatini, Patrick Makwalu amemshukuru msaada uliotolewa na Spika wa Bunge kupitia Taasisi yake ya Tulia Trust kwa kuchangia usafiri ,Jeneza na mahitaji mengine kusaidia msiba huo.

“Hii sio mara ya kwanza kwa Spika kupitia Taasisi yake kugusa jamii lakini pia kwa Marehemu amefanya mambo makubwa ikiwepo kuboresha makazi ambayo yalikuwa sio salama ,kununua kiti mwendo, godoro blanketi na  nguo za kumsitili akiwa hai.”amesema.

Mkazi wa Mtaa wa Kisunga, Godfrey Nyilenda amesema kuna kila sababu ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia vikao vya bunge kuwasilisha Serikali ombi la wananchi itungwe sheria ya kuwachukulia hatua familia zinazotelekeza  wazazi kwa  kutowapatia huduma za msingi wanapofikia uzeeni.