Msuya: Tuchukue hatua thabiti kupambana na corona

Waziri mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa Chama cha mapinduzi, Wilaya ya Mwanga. Picha na Florah Temba.

Muktasari:

  • Waziri mkuu mstaafu Cleopa Msuya, amesema zisipochukuliwa hatua thabiti za kupambana na corona, yanaweza kutokea maafa makubwa.

Mwanga. Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya amesema kama hatua thabiti za kupambana na ugonjwa wa corona hazitachukuliwa, yanaweza kutokea maafa makubwa.

 Msuya ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 24, 2021, wakati akitoa hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

"Naomba tukumbushane maelekezo ya serikali ya awamu ya sita juu ya mchakato wa kupambana na gonjwa hili la corona, gonjwa hili limetikisa dunia nzima na limeendelea kusambaa,"

"Tanzania tumeathirika kwa kiasi, lakini kama hatua thabiti hazitachukuliwa maafa makubwa yanaweza kutokea, tufuate maelekezo yanayotolewa na viongozi pamoja na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka au kutumia sanitizer pamoja na kuepuka misongamano,"amesema.

Vilevile amesema kanuni hizo za kujikinga na kujilinda na corona, pia ziendelee kuzingatiwa katika nyumba za ibada, mashuleni, vyuoni, nyumbani na kwenye vyombo vya usafiri.

Msuya ameutaka mkutano mkuu huo, kutoa tamko la kuomba viongozi wa nyanja zote kushawishi wananchi kuchukua tahadhari na kutekeleza hatua zote za kujikinga na ugonjwa huo hatari na kusisitiza mtu ambaye hatazingatia hatua za kinga atapata maafa.

"Nchi nyingi duniani zimetikiswa na gonjwa hili, sisi sio kisiwa, hivyo Tanzania kama moja ya jamii duniani, inashiriki kwenye maelekezo haya kwa wananchi wake, viongozi wametoa na wameendelea kushauri la kufanya ili kuepukana na janga hili la corona, wananchi itikeni wito huu kwa vitendo."

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi amesema suala la kuchukua tahadhari ya corona lisiwe jambo la kubembelezana.

"Tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya corona, tuepuke misongamano, tuvae barakoa na kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na suala hili la kuchukua tahadhari, isiwe jambo la kubembelezana tena,"amesema Boisafi.