Mtaala kujumuisha elimu ya dini mbioni

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati) akizindua kitabu cha kwanza cha Mwanafunzi cha Elimu ya Dini ya Kiislamu na Makabidhiano ya Muhtasari yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. (kushoto) Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuber na (kulia) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua chombo kitakachosimamia elimu ya dini ya Kiislamu shuleni sambamba kitabu cha elimu hiyo, kilichoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu  Tanzania (Bakwata), ikishirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amezindua kitabu cha elimu ya dini ya Kiislamu kitakachotumika kufundishia elimu hiyo kuanzia mwakani.

Uzinduzi huo umefanyika Novemba 30, 2023 unakuja baada ya majadiliano kati ya wizara hiyo na Bakwata, kuhusu ufundishwaji wa somo la dini ya Kiislamu katika mtaala mpya, jambo lililoifanya taasisi hiyo kutunga kitabu hicho.

Sambamba na uzinduzi wa kitabu hicho pia kimezinduliwa chombo kitakachosimamia mtaala mzima wa elimu ya dini ya Kiislamu shuleni, kinachoitwa Tanzania Islamic Studies Teaching Association (Tista).

Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika  Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, Dar es Salaam, Profesa Mkenda ameisifu Bakwata kutekeleza mchakato huo.

"Wote mnajua tumekamilisha sera ya elimu na uandaaji wake umekuwa shirikishi. Suala la sera ni kama farasi na mtaala ni mkokoteni hivyo sera inavuta mtaala. Masomo ya dini ni ya kipekee hivyo hata mtaala wake si kama masomo mengine hii  ina hisia," amefafanua.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zuberi amesema yote waliyozindua yameshirikisha waislamu wote wa Bara na Visiwani.

"Vyote vimebeba taswira na michango yao naiomba Serikali wafanyie kazi mapendekezo tuliyoyatoa ikiwemo somo lifundishwe na walimu wa Kiislamu, liwe sawa na masomo mengine pamoja na taasusi ya Kiislamu," amesema.

Sambamba na pendekezo hilo mambo mengine yaliyoelezwa na Bakwata ni kuwa na tahasusi maalumu ya dini kwa ngazi ya elimu ya kidato cha tano na sita na Serikali iajiri walimu wa dini ya Kiislam watakaofundisha somo hilo.

Awali Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Mruma alisema mapendekezo hayo yametokana na kamati maalumu iliyoundwa na wizara hiyo kwa ajili ya kukusanya maoni kupitia vyombo mbalimbali vya Kiislam.

Amebainisha kuwa kitabu kilichozinduliwa kinatarajiwa kutumika kuanzia 2024 na kupitia mapendekezo hayo, Serikali inawajibika kugharamia somo la dini shuleni; lengo likiwa ni kuwezesha uimarishwaji wa maadili.

"Hatuna shaka kuwa Serikali itatekeleza maoni na mapendekezo hayo ya wanadini na kuepuka malengo mengine yasiyo mema," amesema na kuongeza kuwa elimu ya dini ya Kiislamu ni mali ya waislamu wenyewe.