Mtaalamu awageuzia kibao wanawake vitendo vya ukatili

Mtaalamu wa masuala ya mahusiano na malezi, Tumsifu Matutu akizungumza na Walimu wanawake wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Askari Polisi Wanawake wa Wilaya ya Misungwi wakati wa kongamano la kuadhimisha Sikukuu ya Wanamke Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Wakati wanaharakati wakiweka nguvu kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, Mtaalamu wa malezi na mahusiano mkoani Mwanza amewageuzia kibao wanawake akidai baadhi yao waliofanikiwa kiuchumi hufanya ukatili dhidi ya wanaume kiasi cha kuwafanya kuzikimbia na kuzitelekeza familia.

Mwanza. Mtaalamu na mshauri wa masuala ya Malezi na Mahusiano, Tumsifu Matutu amesema vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume vinavyofanywa na baadhi ya wanawake waliofanikiwa kiuchumi husababisha waume kuzikimbia na kuziteleteza familia.

Akizungumza kuhusu malezi na mahusiano wakati wa kongamano maalum la wanawake wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Misungwi la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Tumsifu amewataka wanawake wenye uwezo kiuchumi kuacha kubeza kufikiria wanajitosheleza na kuanza kupuuza nafasi za wanaume katika familia.

“Wimbi la vitendo vya ukatili kutoka kwa wanawake wenye uwezi wa kiuchumi sasa limeanza kugeukia kwa wanaume ambao kwa bahati mbaya hawana watetezi kutokana na wanaharakati wengi kuelekeza nguvu nyingi kutetea haki za wanawake. Tunapoadhimisha siku ya Wanawake ni lazima pia tukumbushane kutambua nafasi ya wanaume katika familia,” amesema Tumsifu

Huku ukumbi ukiwa umetulia kumsikiliza, mtaalamu huyo amesema baadhi ya wanawake pia hutumia vibaya maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii siyo tu kwa kuposti picha zinazosababisha ukatili wa kisaikolojia dhidi ya wanaume, bali pia zinazoweza kusambaratisha familia au kusababisha mpasuko katika ndoa.

"Wanawake tunavaa nguo za nusu uchi…kutwa nzima mwanamke yuko kwenye mitandao ya kijamii; hatuna muda wa kuangalia familia. Mume anarejea nyumbani huna muda naye halafu unatarajie usikumbane vitendo vya ukatili. Lazima tubadilike sisi ndipo tutawabadilisha wengine," amesema Mtaalamu huyo

Amesema hata kushamiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto ni matokeo ya baadhi ya wanawake ambao ndio walinzi wa kwanza wa familia kushindwa kutekeleza wajibu wa malezi na makuzi kwa watoto.

“Wanawake turejee katika misingi ya malezi na makuzi kwa familia kwa mujibu wa mila na desturi zetu ndipo tutatokomeza vitendo vya ukatili na kudumisha ndoa zetu," amesema Tumsifu akiwaasa wenzake

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha ameunga mkono hoja ya hiyo akiwasihi wanawake syo kuwa mstari wa mbele kupiga vita vitendo vya ukatili, bali pia nao wasiwe sehemu ya kuwafanyia ukatili wengine.

"Wapo baadhi ya wanawake wanafanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wengine hadi mtu unajiuliza iwapo kweli nao wamezaa na wana watoto. Kila mmoja katika nafasi na eneo lake apige vita ukatili ndipo tutaona mafanikio ya kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani,” amesema Chacha

Mwenyekiti wa Walimu Wanawake Mkoa wa Mwanza, Rachel Matinde amewataka walimu wote nchini kuongoza vita dhidi ya ukatika kwa watu wote kuanzia kwa wanawake, wanaume na watoto.

"Kila tunapokutana kila mtu ajiulize ni kwa jinsi gani vitendo vyake havisababishi ukatili kwa mwingine. Tufanye hivyo ndipo tutajenga Taifa lisilo na makovu ya ukatili,” amesema mwalimu Rachel

Katibu wa CWT Wilaya ya Misungwi, Peresia Manyama amewataka wanawake zaidi ya 100 walioshiriki kongamano hilo kutoka CWT, Jeshi la Polisi na Mahakama kila mmoja kumfunda mwenzake warejeapo majumbani kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa katika jamii.

Amewashauri wanawake waliofanikiwa kiuchumi kutojisahau katika jukumu la malezi, makuzi, ulinzi na ujenzi wa mahusiano na familia bora.