Mtaka akomaa wafanyabiashara kushusha mizigo Soko la Ndugai

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amekazia uamuzi wa Jiji la Dodoma kuhusu wafanyabiashara kushushia mizigo yao katika Soko Kuu la Ndugai, kwamba lazima uheshimiwe na hakuna kubadilisha.

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amekazia uamuzi wa Jiji la Dodoma kuhusu wafanyabiashara kushushia mizigo yao katika Soko Kuu la Ndugai, kwamba lazima uheshimiwe na hakuna kubadilisha.

Kauli ya Mtaka inakuja kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu soko hilo wakisema liko mbali na mji wa Dodoma kwa hiyo wangetamani uamuzi huo ubatilishwe na mizigo ishushwe katika soko kuu la Majengo lililoko mjini kati.

Akizungumza kwenye eneo linalojengwa soko la wafanyabiashara ndogondogo Machinga (Machinga Complex), Mtaka amesema uamuzi wa kushusha mizigo yote katika soko la Ndugai utabaki kama ulivyo lakini akatahadharisha kuwa wafanyabiashara wanaokataa kwenda huko kwa sasa watajutia maamuzi yao baada ya miaka miwili.

Soko la Ndugai limejengwa Nzuguni ambako ni umbali wa kilomita 8 kutoka katikati ya Jiji karibu na stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani lakini limekuwa likilalamikiwa kuwa halina msaada kwa wafanyabiashara kutokana na umbali wa jinsi lilivyojitenga.

Hivi karibu Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza wakurugenzi kutafuta hatima ya masoko yote yaliyojengwa mbali na miundombinu ya wafanyabiashara na akasema wakishindwa basi wageuze kuwa kumbi za burudani na harusi.

“Kwa Ndugai hakuna mjadala, lazima watu wakashushie mizigo yao huko na kuleta mjini, haiwezekani ukaagiza mzigo kutoka Iringa halafu useme kushushia kule ni kuongeza gharama. Kule kuna watu na lazima tufanye hivyo,” amesema Mtaka.

Kuhusu Machinga Complex, mkuu wa mkoa amewapongeza ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kwa ubunifu wa jinsi ya kupata fedha Sh70 bilioni kutoka mapato ya ndani na kuanza ujenzi huo bila kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.

Machinga ya Dodoma Complex inajengwa kwa mapato ya ndani ya Jiji kwa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani na inatarajia kufunguliwa Machi 17, 2022 huku eneo likilenga kuchukua Wamachinga 5,000 ingawa waliosajiliwa hadi sasa ni 3,315.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema mbali na kujenga kwa kutumia fedha za ndani, lakini wametenga maeneo 41 ndani ya Jiji ambayo yatatumika kwa ajili ya wafanyabiashara kwenye mitaa mbalimbali.

Mafuru amesema hadi sasa mkandarasi ameshakabidhiwa Sh841 milioni kwa ajili ya kazi hiyo na wanamtaka afanye kazi kwa haraka ili alipwe fedha zake nao waanze kuwaingiza Wamachinga kwa utaratibu waliojiwekea.