Mtendaji Serikali ya mtaa auawa, watatu wakamatwa

Tuesday October 12 2021
auapic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya ofisa mtendaji wa Serikali ya mtaa wa Mbezi Msumi, Kelvin Mowo (38).

Tukio hilo limetokea saa 11:54 asubuhi jana Jumatatu Oktoba 11, 2021 huko eneo la Msumi Mbezi Wilaya ya Ubungo katika ofisi za Serikali ya mtaa.

Kwa mujibu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, marehemu akiwa ofisini kwake anasikiliza mgogoro wa ardhi ghafla watu  wanne waliingia ofisini na mmoja  akatoa panga na kumshambulia mtendaji huyo kitendo kilichopelekea kupata majeraha makubwa na baadaye akapoteza maisha wakati akikimbizwa hospitali.

“Marehemu ni mkazi wa Bunju. Hivyo watu watatu wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo wanahojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.Majina ya watuhumiwa hao kwa sasa yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi,” amesema Muliro.

Advertisement