Mtobesya aahidi mambo lukuki TLS

Friday May 13 2022
mtobesyapiic
By Juma Issihaka

Dar es Salaam. Suala la Katiba Mpya limechomoza katika kampeni za urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), baada ya mgombea wa nafasi hiyo, Jeremiah Mtobesya kuahidi kuwa atakapochaguliwa chama kitashiriki midahalo ya kulifanikisha hilo.

Mbali na Katiba Mpya, vipaumbele vyake vingine ni kutunisha mfuko wa chama hicho ili kiwe na uwezo wa kifedha, kusaidia mawakili wadogo kupata soko na uhuru na haki ya wanasheria kutekeleza majukumu yao bila bughudha.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, mwanasheria huyo alisema suala la Katiba Mpya limo ndani ya mpango kazi wa TLS wa mwaka 2020/22 na atakachokifanya ni kuutekeleza.

“TLS inaongozwa na mpango kazi. Mpango kazi wa mwaka 2020/22 vitu vingi vimeelezewa. Pamoja na mambo mengine, kuna kipengele kinasema chama kitashiriki midahalo ya kuisaidia nchi kupata Katiba,” alisema.

Kuhusu uongozi wake, alisema utafanya na kushiriki mijadala na midahalo kuhusu mabadiliko ya katiba kwa kuwa ni jambo lililoridhiwa na wanachama wote wakati wa kuandaa mpango kazi huo jijini Arusha mwaka 2020.

“Mimi nitakuwa muumini wa kufuata makubaliano yaliyopo katika mpango kazi, sitaingia kufanya ya kwangu, nitafanya tuliyokubaliana,” alisema Mtobesya.

Advertisement

Kuhusu kipaumbele cha kutunisha mfuko wa TLS, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja chama hicho kimepitia hali ngumu ya kiuchumi.

Mtobesya alisema ukata huo umesababisha kukwama kwa utekelezaji wa baadhi ya majukumu yenye masilahi kwa chama hicho.

Kuhusu vyanzo vya mapato alisema vinatokana na ada za wanachama kila mwaka na za mafunzo endelevu zilizopunguzwa na kuanzishwa vyanzo vingine vitatu vya mapato.

Alivitaja vilivyoanzishwa kuwa ni idara ndani ya sekretarieti yenye wajibu wa kutafuta fedha kwa wahisani na mbinu nyingine, kuanzisha taasisi ya mafunzo kwa wanasheria na taasisi nyingine inayoongeza mapato, lakini kati ya hizo ni moja ndiyo inayofanya kazi hadi sasa.

“Hivi vitu vitatu ilikuwa vyote vitusaidie kuongeza mapato kuziba mwanya wa punguzo la ada za wanachama. Idara mbili ile ya mafunzo na ya kukusanya fedha hazifanyi kazi, mimi nikiingia nitahakikisha zinafanya kazi kuongeza mapato,” alisema.

Mwanasheria huyo alisema kipaumbele kingine ni kutengeneza mfumo wa kuwawezesha wanasheria wadogo kuendana na soko.

Atakapochaguliwa, alisema TLS haitafanya kazi zake kimyakimya, bali itatoa tafsiri katika kila jambo linalostahili maana ya kisheria na kupinga yasiyostahili.

“Uongozi uliopo sasa hivi nimesikia watu wanasema mfumo wa uendeshaji wa shughuli za uongozi kuna vitu havistahili kusemwa hadharani au kutoa matamko kila wakati na inaamuliwa kufanya kimya kimya, lakini wakati wangu nitasema hadharani,” alisema.

Advertisement