Mtwara waomba kukamilishiwa barabara vijijini

Ujenzi wa barabara ya Nanyamba Nitekela Nyundo ukiendelea

Muktasari:

Wakati msimu wa korosho wa 2022/23 ukikaribia, baadhi ya wananchi mkoani Mtwara wameomba kukamilishiwa bara za vijijini.

Mtwara. Wananchi wa Kata ya Nyundo katika Halmashauri ya mji wa Nanyamba wamemuomba Mkandarasi anaejenga barabara ya Nanyamba Nitekela Nyundo kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuwahi msimu wa korosho.

Msimu wa korosho 2022/2023 unatarajia kuanza mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo asilimia 70 ya zao hilo hulimwa mkoani humo.

Mradi wa ujenzi wa kilometa moja ya barabara ya Nanyamba, Nitekela Nyundo unaogharimu Sh849.9 milioni ulianza Oktoba, 2021 na unatarajia kukamilika Agosti 30, mwaka huu.

Mkazi wa Kijiji cha Nitekela, Melckzedeck Wilbroad ameiambia Mwananchi Digital leo Jumatano Agosti 11, 2022 kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji ikiwemo wa zao kuu la uchumi mkoani hapa, korosho.

Katika msimu huu jumla ya tani 400,000 za korosho zinatarajia kuzalishwa nchini kote.

"Kipande hiki kikikamilika ni ukombozi kwetu kwa sababu kama unavyopaona hapa pana mlima mkali, wakati wa mvua hapapitiki inabidi kusubiri mpaka pakae sawa hivyo kuchelewesha mazao sokoni," amesema Willbroad.

Kwa upande wake Muhibu Athumani wa Kijiji cha Niumba amesema kukamilika kwa mradi huo ndani ya wakati ni ukombozi mkubwa kwao hivyo Mkandarasi atilie maanani suala hilo.

"Kujengwa kwa barabara hii tunashkuru ikikamilika kwa wakati maana sisi wakazi wa Kata hii ya Nyundo tunaitegemea sana kusafirisha mazao yetu," amesema Athumani.

Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Mkandarasi kutoka kampuni ya Safi Group Company Limite, Mhandisi Makongoro Julius amesema mradi kwa sasa umefikia asilimia 70 na hakuna changamoto yoyote hadi sasa hivyo ni matumaini yake kwamba utakamilika kwa wakati.


Naye Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini, (Tarura), Mhandisi Karim Ahmad amesema hadi sasa Mkandarasi huyo ameshalipwa Sh293.5 milioni kati ya Sh850 za mradi wote.

"Hakuna changamoto yoyote zaidi ya milima mingi iliyopo eneo hili na hali ya hewa hasa kipindi cha mvua inayotufanya tuwe makini zaidi na utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake Katibu tawala Wilaya ya Mtwara, Thomas Salala amesema, "Tumeridhika na utekelezaji wa mradi, tunachokitana ni Tarura na Mkandarasi kukamilisha mradi ndani ya muda unaotakiwa.”