Muda vifungashio vya plastiki wafikia kikomo

Muda vifungashio vya plastiki wafikia kikomo

Muktasari:

  • Ikiwa leo ni siku ya mwisho kwa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyo na viwango wala ubora, wajasiriamali wadogowadogo ambao ni watumiaji wake wamesema hawafahamu chochote na wanaendelea kuvitumia kama kawaida.

Dar es Salaam. Ikiwa leo ni siku ya mwisho kwa matumizi ya vifungashio vya plastiki visivyo na viwango wala ubora, wajasiriamali wadogowadogo ambao ni watumiaji wake wamesema hawafahamu chochote na wanaendelea kuvitumia kama kawaida.

Januari 8, 2021 aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu alitoa muda wa miezi mitatu kuondoa vifungashio hivyo.

Gazeti la Mwananchi lilitembelea maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam ikiwemo soko la Kariakoo, Temeke, Ilala na Buguruni na kujionea watu wakiendelea kutumia vifungashio hivyo huku wakidai hawafahamu kama Serikali imetoa katazo hilo.

Mariam Athumani, muuzaji wa nyanya katika soko la Temeke alisema hajui kama Serikali ilitoa muda hadi kesho kutumia vifungashio hivyo.

“Ndio kwanza kama ninavyokusikia wewe, kiukweli tutapata shida kwa kuwa mifuko hii ilikuwa inatusaidia kuwafungia wateja wakija kununua nyanya na vitu vingine vidogovidogo,” alisema Mariam.

Muda vifungashio vya plastiki wafikia kikomo

Pia Hamidu Ramadhan, muuzaji wa vifungashio hivyo maeneo ya Soko la Ilala alisema alikuwa hajui kama kuna ukomo wa matumizi ya vifungashio hivyo, lakini akasema kama kuna utaratibu huo watakuwa tayari kufuata muongozo uliotolewa.

“Ingawa nitapata shida kwa kuwa maisha yangu yanategemea kuuza vifungashio hivi, hatuwezi kupingana na Serikali,” alisema.

Alisema fungu moja la vifungashio hivyo ananunua kwa bei ya jumla kwenye soko la Kariakoo kisha anawauzia wateja wake kwa Sh500 ambapo ndani yake kunakuwa na vifungashio 30.