Muliro: Bado asilimia 13 kudhibiti panyarodi Dar

LIVE: Jitihada za Polisi kudhibiti 'Panyaroad'

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kwa tathimini yake, jeshi hilo limefanikiwa kudhibiti vikundi vya uhalifu maarufu panyaroad kwa asilimia 87, huku likiendelea kutafuta asilimia 13 ya waliotoroka.

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kwa tathimini yake jeshi hilo limefanikiwa kudhibiti vikundi vya uhalifu maarufu panyaroad katika jiji hilo kwa asilimia 87.

Amesema kuwa wanaendelea kufuatilia asilimia 13 ya vikundi vya uhalifu hasa kwaa waliokimbia kwenye maeneo baada ya Jeshi hilo kufanya msako katika maeneo yanayotambulika.

Amebainisha kuwa lengo ni kufanikiwa kudhibiti vikundi hivyo kwa asilimia 100 hivyo bado wanaendelea kusaka wahalifu wengine katika jiji hilo.

Kamanda Muliro amebainisha hayo leo Jumatatu Oktoba 3, 2022 wakati wa mjadala kitaifa juu ya hali ya kiusalama na jitihada za Jeshi la Polisi katika kudhibiti panyarodi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha na Dodoma ulioandaliwa na Watch Tanzania ambao umefanyika kupitia mtandao wa zoom.

Pamoja na maelezo mengine, muongoza mjadala huo alimuuliza Kamanda huyo kuwa operesheni za kuwakamata panyaroad kwa jiji la Dar es salaam zimefanikiwa kwa asilimia ngapi.

Akijibu swali hilo, Kamanda Muliro amesema “Mimi nikiulizwa leo kwamba imefanikiwa kwa asilimia ngapi, nakuambia imefanikiwa kwa asilimia 87.

“Kwa sababu 13 bado kuna makundi baada ya hekaheka dhidi ya makundi haya, kwa kufuatilia nyumba kwa nyumba, mitaa kwa mitaa baadhi yao wametoroka kwenye maeneo tunayoyatambua

“Kwa hiyo Asilimia 87 tumefanikiwa, hii 13 bado tunaendelea nayo mpaka wananchi wasahau hili suala linaloitwaa panyaroad au masuala mengine ya kihalifu ili warudi katika shughuli zao za kawaida za kiuchumi, kisiasa pamoja na kijamii,” amesema Kamanda Muliro.

Kuhusu waliotoka magerezani na kujihusisha na makundi ya panyarodi, amesema miongoni mwa vijana 10 wanaokamatwa kwa watatu wanakuwa wametoka magerezani.

“Uko uhusiano wa karibu kwa sababu kati ya makundi tunayoyakamata na kuyapeleka mahakamani unakuta kwenye kundi kati ya watu 10 wamo watu watatu ambao wameshapita kwenye mifumo hii ya kisheria, kwa maana waameshapita Polisi, mahakamani wakaendaa mahabusu au magereza wakatoka kwa sababu mbalimbali za kisheria.

“Wakirudi wanajiunga kwa kutumia watu wengine wapya, kwa hiyo rekodi ya watu wa zamani inaungakjina na watu wapya, unakuta wanatenda tendo la kihalifu,” amesema.