Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mume jela miaka 12 kwa kumuua mkewe bila kukusudia

Muktasari:

  • Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dodoma, imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela Issa Khalfan maarufu Mashori, baada ya kukiri kumuua mkewe bila kukusudia. Chanzo cha mauaji ni mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia uliosababishwa na jaribio la kuuza nyumba ya familia.

Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dodoma, imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela Issa Khalfan baada ya kukiri kosa la kumuua bila kukusudia mkewe, Hawa Yusuph Madai, kutokana na mgogoro wa kifamilia uliodumu kwa muda mrefu.

Mauaji hayo yalitokea Novemba 19, 2023 katika eneo la Mwaja, Kata ya Mandewa, Tarafa ya Unyanyembe mkoani Singida, ambapo Issa alimuua mkewe kwa kumkaba shingoni.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Evaristo Longopa Juni 5, 2026, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Mahakama ilielezwa kuwa tukio la mauaji lilitokea usiku wa Novemba 19, 2023 baada ya mzozo kati ya wanandoa hao kuhusu mpango wa kuuza nyumba na ardhi ya familia.

Ilielezwa kuwa marehemu Hawa alikuwa akipinga mpango huo kwa sababu familia haikuwa na makazi mbadala, jambo lililosababisha migogoro ya mara kwa mara kati yake na mumewe.

Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, ilibainika kuwa mwaka 2018 mshtakiwa alimshambulia mke wake na kumvunja mkono.

Aidha, siku chache kabla ya tukio la mauaji, kati ya Novemba 15 na 16, 2023, alijaribu pia kumnyonga, lakini mkewe aliokolewa baada ya kupata msaada na kufanikiwa kutoroka.

Mahakama ilieleza kuwa vitendo hivyo vilionesha kuwepo kwa historia ya unyanyasaji wa nyumbani kabla ya tukio lililosababisha kifo.

Kwa mujibu wa taarifa za kesi, usiku wa tukio mshtakiwa alimshambulia mke wake akidai alikuwa kikwazo katika mpango wake wa kuuza mali za familia. Wakati wa ugomvi huo, Hawa alijaribu kujitetea, lakini alizidiwa nguvu na mshtakiwa ambaye alimkaba shingoni kwa nguvu kubwa hadi kupoteza maisha.

Ripoti ya uchunguzi wa kitabibu ilibainisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa ukosefu wa oksijeni kwenye ubongo uliosababishwa na kunyongwa. Mwili wa marehemu haukuwa na majeraha mengi yanayoonekana kwa nje.

Aidha, wataalamu walichukua sampuli kutoka kwenye shingo ya marehemu pamoja na sampuli za mate kutoka kwa mshtakiwa kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa DNA iliyopatikana kwenye shingo ya marehemu ililingana na DNA ya mshtakiwa, jambo lililosaidia kuimarisha ushahidi dhidi yake.

Baada ya mahakama kumtia hatiani, wakili wa Serikali aliomba mahakama kutoa adhabu kali akieleza kuwa marehemu alikuwa mama wa watoto watatu na alikuwa akijitahidi kulinda maslahi ya familia yake.

Amesema hakuna sababu iliyohalalisha mshtakiwa kumuondolea maisha mke wake kwa sababu tu ya kutokubaliana kuhusu uuzaji wa nyumba ya familia.

Pia alisisitiza kuwa mshtakiwa alikuwa ameonyesha nia ya kutaka kumuua marehemu kutokana na matukio ya awali ya kumnyonga na kumtishia maisha.

Kwa misingi hiyo, upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutoa adhabu itakayokuwa fundisho kwa jamii dhidi ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na unyanyasaji wa majumbani.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi aliomba mahakama impe adhabu nafuu mshtakiwa akieleza kuwa hana rekodi ya makosa ya awali, ana umri wa miaka 58 na anategemewa na watoto sita pamoja na mama yake mwenye umri wa zaidi ya miaka 80.

Aidha, amesema mshtakiwa alikuwa ameshatumikia miaka miwili na nusu gerezani akiwa mahabusu tangu alipokamatwa na kuwa baada ya tukio hakukimbia wala kujificha, bali aliwajulisha watoto wake na majirani kuhusu kilichotokea, jambo ambalo kwa maoni yake lilionesha ushirikiano na vyombo vya sheria.


Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji Longopa amesema mahakama hukumu ya juu kabisa ya kosa hilo inapaswa kuwa kifungo cha maisha, ila mahakama inapewa mamlaka kutoa adhabu kulingana na hali ya kesi husika.

Mahakama ilibaini kuwa historia ya kumpiga mkewe hadi kuvunjika mkono, pamoja na majaribio ya awali ya kumnyonga, ilikuwa ushahidi wa wazi wa unyanyasaji wa nyumbani uliodumu kwa muda mrefu.

“Mahakama hii inaona kuwa kifo cha marehemu kilitokana na mwenendo wa muda mrefu wa unyanyasaji wa nyumbani uliofanywa na mshtakiwa dhidi ya mwathiriwa,” amesema Jaji Longopa katika sehemu ya hukumu.

Kutokana na uzito wa mazingira hayo, mahakama ilisema adhabu ya msingi inayostahili ilikuwa kifungo cha miaka 17 jela.


Kwa mujibu wa mahakama, miaka miwili na nusu ilipunguzwa kutokana na kukiri kosa na sababu nyingine za kibinadamu, huku miaka mingine miwili na nusu ikipunguzwa kutokana na muda aliokuwa amekaa mahabusu.

Baada ya kupunguza muda huo, mahakama ilibakiza kifungo cha miaka 12 kuwa adhabu inayofaa kwa mshtakiwa.

“Mahakama inaona kuwa kifungo cha miaka 12 kinatosha kuonesha uzito wa kosa hili, hivyo inamhukumu Issa adhabu hiyo kuanzia leo,” amesema Jaji.