Museveni: Mkataba wa bomba la mafuta sawa na  'ushindi wa tatu' kwa Tanzania na Uganda

Muktasari:

  • Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema utiaji saini mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani Tanzania (EACOP), ni ushindi wa tatu kwa nchi hizo mbili kwa kuwa tarehe hiyo ina kumbukumbu kubwa.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema utiaji saini mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani Tanzania (EACOP), ni ushindi wa tatu kwa nchi hizo mbili kwa kuwa tarehe hiyo ina kumbukumbu kubwa.

Museveni ametoa kauli hiyo leo Jumapili Aprili 11, 2021 wakati wa hotuba yake mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,  wakati  wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa  bomba hilo.

 Amesema miaka 42 iliyopita, siku kama ya leo  wanajeshi wa Tanzania chini ya Jenerali David Msuguri, waliteka Kampala na kumwezesha ofisa wa jeshi la Uganda David Oyite Ojok kutangaza kuanguka kwa Idi Amin kwenye Redio Uganda.

“Wakati huo huo nikiwa na  vikosi vyangu vya Fronasa kwenye mkondo mwingine chini ya Meja Jenerali Cyrus Mayunga huko Mbarara. Leo, kwa hivyo, ni ushindi wa mara tatu kwa Tanzania na Uganda,” amesema.

Museveni amesema kuwa ushindi wa leo ni ushindi wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, baada ya ushindi wa awali wa kijeshi na kisiasa kupatikana.


“Katika nyakati hizi mbili,  Mwalimu Nyerere alikuwa mtu muhimu sana kwetu.  Mnamo mwaka  1978-79, JWTZ ilichukua jukumu kubwa katika kumuondoa Idi Amin. Kuanzia  1985 hadi 1986, Mwalimu Nyerere alitupa bunduki 5,000 kwa wakati mwafaka kabla tu ya shambulio la Kampala kuanza tarehe 17 Januari 1986,” amesema

Kuhusu uhusiano wa Uganda na Kenya, amesema nchi hizo mbili ni za kindugu, kama Tanzania, hata hivyo, kihistoria kuna nafasi ya kipekee kwa Tanzania linalomfanya ahisi kuwa ana deni.

“Kwa hivyo nimeridhika zaidi kuwa mradi huo utatoa mchango kiasi fulani katika maendeleo ya Tanzania. Hata hivyo,  haiwezi kulipa fidia kubwa ambayo Tanzania ilitoa katika kumuondoa Idi Amin na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika kama Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini. Ni mchango wa kawaida tu, "amesema.