Musukuma adai usomi wa Profesa Muhongo hauna faida kwa Tanzania

Musukuma adai usomi wa Profesa Muhongo hauna faida kwa Tanzania

Muktasari:

  • Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma amemshukia  mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo kwamba usomi wake hauna faida kwa Tanzania.

Dodoma. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma amemshukia  mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo kwamba usomi wake hauna faida kwa Tanzania.

Musukuma amesema ni wakati kwa Serikali kuwaamini wasomi aliowaita wa darasa la saba akidai kuwa wanakulia kwenye kazi.

Mbunge huyo ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo jioni Jumanne Aprili 13, 2021 katika mjadala wa mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu mwaka 2021/22.

Amebainisha kuwa ni wakati wa Serikali kuwaamini watu wenye elimu ya darasa la saba badala ya kung'ang'ania maprofesa wasiokuwa na maana ambao wakati wote wanasubiri wengine waanzishe halafu wao wabebee ajenda juu kwa juu.

Amemtaja Profesa Muhongo kwamba wakati akiwa waziri wa nishati na  madini alishindwa kufanya mambo mazuri lakini anashangaa kuona ameanza kuwa mkosoaji mkubwa.

"Mwaka 2016 nilimuita Profesa Muhongo nikamwambia kwenye haya makinikia tunaibiwa lakini alichukua kipaza sauti akatangaza hadharani kwamba Geita wamechagua mtu wa darasa la saba wamekosea sana," amesema Msukuma.

Amesema baada ya hapo walichukua mchanga wakaenda nao mbele ya rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli na ilibainika kuwa mchanga huo ulikuwa na madini ya thamani kubwa.

Musukuma adai usomi wa Profesa Muhongo hauna faida kwa Tanzania

Aprili 9, 2021 bungeni mjini Dodoma, Profesa Muhongo alisema uchumi wa gesi pekee ndiyo utakaoifikisha Tanzania kwenye uchumi thabiti na kukosoa  mawazo ya kutegemea uzalishaji wa umeme mkubwa kwa kutumia maji.

Amesema Tanzania inatakiwa ijikite katika matumizi ya umeme mchanganyiko badala ya kutegemea mabwawa ya maji ambayo wakati wowote yanaweza kukauka.