Mutafungwa awaonya madereva wanaovunja sheria barabarani

Muktasari:

  • Kamanda Mutafungwa ametembelea eneo la ajali iliyosababisha vifo vya watu 20 mkoani Shinyanga na kutoa onyo kwa madereva wanaovunja sheria za barabarani

Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabaranii, Wilbroad Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu madereva wanaovunja sheria na kutofuata taratibu za usalama barabarani.

Mutafungwa ameyasema hayo leo alipotembelea kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga eneo ambalo ajali iliyoua watu 20 imetokea.

Ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Agosti 9, 2022 imesababisha vifo vya watu 20 na wengine 15 kujeruhiwa ambapo ajali hiyo iliyohusisha magari matatu.

Akizungumza akiwa katika eneo hilo, Mutafungwa amesema hatua ya kuwachukulia hatua madereva watakaovunja sharia za barabarani inalenga kudhibiti ajali zinazotokea kila mara na kugharimu maisha ya watanzania wengi.

“Kwenye hiyo gari aina ya Hiace taarifa ni kwanba dereva alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi, eneo hili tayari kulikuwa na ajali hivyo alitakiwa kuchukua tahadhari za kutosha ila hakufanya hivyo.

“Kingine madereva wanatakiwa kufahamu kuwa unapoendesha chombo cha moto unatakiwa kujiweka mbali na ulevi. Usitumie kinywaji halafu ukaenda kuendesha gari,” amesema

Kamanda Mutafungwa pia alitoa agizo kwa wamiliki wa matrekta kuweka viakisi mwanga ili kuonekana kwa urahisi yanapokuwa barabarani wakati wa usiku.

Hadi kufikia jioni ya leo miili 16 kati ya 20 iliyopelekwa katika hospitali ya wilaya Kahama ilitambuliwa na kuchukuliwa na wahusika.