Mvua yakata mawasiliano kati ya Ifakara na Mlimba Morogoro

Barabara iliyokatika baada ya kalavati linalounganisha Barabara ya Ifakara-Mlimba kusombwa na maji jana Aprili mosi, 2024.  Picha na Johnson James

Muktasari:

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Morogoro,   Alinanuswe Kyamba amesema jitihada za kurejesha mawasiliano zinaendelea

Morogoro. Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro zimesababisha kukatika kwa barabara inayounganisha Ifakara na Mlimba baada ya kusombwa kwa kalavati linalounganisha pande hizo mbili.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 2, 2024 kuhusu uharibifu huo uliotokana mvua zilizonyesha jana Jumatatu Aprili mosi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Morogoro,   Alinanuswe Kyamba amesema jitihada za kurejesha mawasiliano zinaendelea.

"Ni kweli Aprili mosi tulipata changamoto ya barabara inayounganisha Ifakara na Mlimba kukatika baada ya kalvati  inayounganisha maeneo hayo kusombwa na maji, ni kweli kwa sasa eneo lile huwezi kupita kutoka upande mmoja kwenda mwingine, hiyo ni kutokana na maji kuwa mengi lakini jitihada za kurejesha hali ya kawaida zinaendelea kutoka kwa wataalamu wetu," amesema Kyamba.

"Tayari timu ya mafundi kutoka mkoani hapa na wale wa Mlimba penyewe,  wameshafika eneo lililokatika na tumeshapeleka mitambo kwa ajili ya kusaidia kuondoa vifusi na mawe ambayo yameziba eneo lile baada ya daraja kusombwa na maji,” amesema Kyamba.

“Nawaomba wananchi wa maeneo hayo wawe watulivu maana tunafanya kazi usiku na mchana kuona hali inarudi kama zamani."

Hata hivyo, Kyamba amesema mvua zilizonyesha kwa mwaka huu ziko juu ya wastani na maeneo mengi Mkoa wa Morogoro yameathirika.

Kyamba amesema Barabara ya Ifakara- Mlimba imeanza kumeguka tangu Januari,  hivyo kinachotokea ni mwendelezo tu maana mvua zimenyesha kwa wingi katika maeneo hayo.

"Barabara ya Ifakara-Mlimba haijaanza kubomoka kuanzia leo, bali barabara imeanza kusombwa na maji tangu Januari mwaka huu, imekuwa ikisombwa na maji tunarekebisha, zaidi ya kalvati tano zimesombwa na tumejenga upya, "amesema Kyamba.

Mwananchi Digital  imemtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, kuzungumzia suala hilo lakini amesema yuko kwenye kikaoni akimaliza atatoa taarifa.

Barabara iliyokatika baada ya kalavati linalounganisha Barabara ya Ifakara-Mlimba kusombwa na maji jana Aprili mosi, 2024.  Picha na Johnson James

Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi alipoulizwa kuhusu barabara ya Ifakara -Mlimba kukatika amesema anaendesha gari kutoka Morogoro kuelekea bungeni jijini Dodoma, akifika atakuwa kwenye wakati mzuri wa kuzungumza.

Mkazi wa Mlimba, Eduard John amesema baada ya mvua kunyesha na kusomba kalavati hakuna anayeweza kuvuka kwenda upande wa Ifakara.

"Barabara hii ilikatika jana baada ya kalvati kusombwa na maji, hali iliyosababisha barabara kumeguka sehemu kubwa baada ya maji kuwa mengi, sasa huku tulipo Mlimba ni kama tuko kisiwani maana hatuwezi kwenda Ifakara tena baada ya barabara kukatika, hata wasafiri nao hawawezi kusafiri maana magari hayawezi kupita kwa kuwa eneo lililokatika ni kubwa na pana," amesema John.

"Ni kweli mvua zimenyesha kubwa, lakini hata barabara nayo ilikuwa nyembamba sana,  kwa hivyo yale maji yalipokuja yakalizidi kalvati na kuondoka nalo, kwa kuwa barabara ilikuwa nyembamba nayo ikasombwa, ndio maana unaona hakuna anayeweza kupita wala kurudi kwa pande zote za Ifakara na Mlimba."

Mkazi wa Ifakara, Salvatory Mwambungu amesema adha wanazopata kutokana na barabara hiyo kukatika hata kwenda kutafuta riziki upande wa Mlimba imekuwa changamoto kwao.

"Kwetu sisi wakazi wa Ifakara mara nyingi kwenda Mlimba tunakwenda kupambana kutafuta riziki, lakini kitendo cha barabara hii kukatika hatuwezi tena kwenda huko maana lile eneo linaonyesha kabisa mpaka ukarabati mkubwa ufanyike ndipo magari na usafiri yapite," amesema.