Mvutano TRC, PPRA zabuni ujenzi SGR

Muktasari:

  • Zabuni ya mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha reli ya kisasa (SGR) imeibua mzozo kati ya taasisi mbili za Serikali.


Dar es Salaam. Zabuni ya mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha reli ya kisasa (SGR) imeibua mzozo kati ya taasisi mbili za Serikali.

Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) linataka kampuni ya Uturuki, Yapi Markezi ichukuliwe kwa kazi hiyo kwa njia moja ya ununuzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ina maoni kwamba mkandarasi apatikane kupitia mchakato wa zabuni wa ushindani.

Kipande cha tatu na nne cha mradi wa SGR kinajumuisha usanifu na ujenzi wa kipande cha reli chenye urefu wa kilomita 533 kutoka Makutopora hadi Tabora na kutoka Tabora hadi Isaka.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Mary Swai hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo. “Mimi sio msemaji wa Serikali ... siko tayari kuzungumzia masuala ya Serikali kwenye vyombo vya habari,” aliiambia Mwananchi jana.

Nyaraka zilizopatikana kwa gazeti hili zinaonyesha kumekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya taasisi hizo, huku TRC ikishinikiza njia moja ya ununuzi.

Katika barua yake ya Julai 23, 2021, TRC inaelezea faida za kutoa zabuni kwa njia ya ununuzi wa chanzo kimoja cha Yapi Markez.

Lakini, katika majibu yake ya Julai 27, 2021, PPRA inakumbusha TRC kwa nini mchakato wa zabuni za ushindani lazima upewe kipaumbele kila wakati.

“Mamlaka ingependa kushauri kwa mujibu wa kifungu cha 64 (1) cha PPA, 2011 na kanuni ya 149 (1) ya PPR 2013, zabuni ya ushindani inapaswa kupewa kipaumbele katika ununuzi wa bidhaa, ujenzi au huduma.

“Kwa msingi huu na kulingana na ushauri wa kina uliotolewa kwenye kiambatanisho kilichoambatanishwa na barua hii, mamlaka inashauri TRC kuzingatia kutumia zabuni ya ushindani katika kupata wakandarasi kwa kipande cha tatu na cha nne,” inasoma sehemu ya barua hiyo.

PPRA, inaeleza barua hiyo, inaamini kupitia mchakato wa zabuni ya ushindani, Serikali itapata thamani ya fedha katika mradi huo.

Kwa mujibu wa PPRA, ilikuwa kupitia zabuni ya ushindani kwamba Serikali iliokoa Dola za Marekani 1.03 bilioni (karibu Sh2.37 trilioni kwa kiwango cha ubadilishaji uliopo) wakati ikitoa zabuni ya ujenzi wa kipande cha tano cha SGR.

Zabuni ya kujenga SGR kutoka Mwanza hadi Isaka ilitolewa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Corporation na China Railways Construction Corporation (CCECC-CRCC) kwa bei ya mkataba wa zabuni ya Dola 1.326 bilioni (pamoja na VAT) wakati mzabuni wa pili wa chini alikuwa Yapi Merkezi aliyekuwa amesahihisha bei ya zabuni ya Dola 2.356 bilioni (karibu Sh5.4 trilioni).

“Ilikuwa tofauti kubwa ya Dola 1,030,068,831.21 na kwa hivyo, Serikali isingeweza kuokoa kiasi hiki endapo ingechagua njia moja ya ununuzi,” inaeleza barua hiyo.

Katika utetezi wake wa chanzo kimoja cha Yapi Merkezi, barua ya Mkurugenzi Mkuu wa TRC ambaye pia ni ofisa masuuli wa shirika hilo, Masanja Kadogosa alisema ingawa bodi ya zabuni (ya TRC) ilikuwa imeshauri mkandarasi wa kipande cha tatu na cha nne achukuliwe kupitia mchakato wa zabuni ya ushindani, ilibidi atafute uhakiki kwa sababu kumchagua Yapi Merkezi kungekuwa na faida kadhaa.

Barua hiyo inabainisha Yapi Merkezi ilikuwa imeaminiwa kufanya kazi hiyo vizuri kwa sababu tayari ilikuwa ikifanya kazi hiyo nchini na tayari ilikuwa ina kiwanda, vifaa na wafanyakazi wake nchini Tanzania.