Mwakibete aiagiza TRC tiketi kielektroniki kwa wote

Wednesday January 19 2022
TRC PIC
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amelielekeza Shirika la reli Tanzania (TRC) kuufanyia kazi mfumo wa ukatishaji tiketi kielektroniki ili kutoa fursa kwa wananchi kuutumia kupata huduma hiyo.

Mwakibete amesema TRC inapaswa kuwa na teknolojia inayoendana na mahitaji ya wateja wake hivyo Watanzania wengi kutokuwa na simu janja haipaswi kuwa kisingizi.

Akizungumza baada ya kufanya ziara kwenye shirika hilo Mwakibete amesema mfumo huo unapaswa kuwafikia watumiaji wote wa usafiri huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa mfumo uliopo sasa unaruhusu wenye simu janja pekee kukata tiketi kwa njia ya mtandao na kulipa nauli kwa mfumo huo.

“Mfumo uliopo unatumia simu janja tunaangalia namna ya kuuoboresha kwa kuwa wateja wetu wengi wako vijijini na hawana smartphone.

“Hii inasababisha usumbufu wakati mwingine wanasafiri umbali mrefu kwenda kwenye vituo vyetu kukata tiketi na wakifika wanaweza kukuta tiketi zimeisha,” amesema Kadogosa.

Advertisement

Akizungumzia hilo, Naibu Waziri amesema suluhisho lake linapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wote wa usafiri huo.

“Nawaelekeza kaeni na timu yenu ya tehama mkalifanyie kazi suala hili, mfumo wa kufanya booking na kukata tiketi unatakiwa uwafikie watu wote wenye simu huko vijijini hawana simu janja,”amesema Mwakibete.

Advertisement