Mwanafunzi akutwa ameuawa kichakani Bukoba

Waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa wanafunzi  Elius Antony (13)  aliyeuawa katika Kitongoji cha Mwizi Wilaya ya  Bukoba. Picha na Ananias Khalula

Muktasari:

  • Mwananfunzi darasa la sita katika Shule ya Msingi Kilima Wilaya ya Bukoba, Elius Anthony (13) amekutwa ameuawa kwa kukatwa panga shingoni na mwili kutelekezwa kichakani.

Bukoba. Mwanafunzi darasa la sita katika Shule ya Msingi Kilima Wilaya ya Bukoba, Elius Antony (13) ameuawa kwa kukatwa panga shingoni na mwili wake kutelekezwa kichakani katika Kitongoji cha Mwizi, Nyakato Wilaya ya Bukoba.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda leo Aprili 13, 2024 akisema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mauaji hayo na ukikamilika watatoa ufafanuzi.

Akizungumzia tukio hilo kijijini hapo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilima, Izidory Kaiza amesema alipokea taarifa za kupotea kwa mtoto kwenye Kitongoji cha Mwizi tangu Aprili 10, 2024 kutoka kwa wazazi wake.

"Tulifuatilia kwa makini hadi kwenye kichaka tukaona nguo na mguu na baadaye mwili wake. Tukawajulisha polisi ambao walifika na gari na vifaa vya kubebea maiti.

“Ndipo wazazi wa mtoto walipoambiwa waje wamtambue mtoto wao, walipomfunua tukaona amefariki na alikuwa amepigwa panga shingoni," amesema Izidory.

Beatrida Anthony, mama mzazi wa marehemu amesema mara ya mwisho mtoto wao alikuwa amekwenda na baba yake kuchoma mkaa porini, baadaye alirudi nyumbani kufuata simu na Sh10,000 kwa ajili ya matumizi.

"Baba yake alipofika hapa nyumbani alipokelewa na salamu za pole kutoka kwa majirani za kupotelewa na mtoto na wakati tunaendelea na mazungumzo mwenyekiti wa kijiji alikuja na pikipiki akambeba baba yake kuelekea huko Mwizi walikoukuta mwili wa mtoto, ukiwa kichakani umejaa na nzi," amesema Beatrida.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilima, Reginah Richard, amesema wamepokea taarifa za mauaji ya kikatili ya mwanafunzi huyo amelaani vikali tukio hilo.