Mwanafunzi auawa akituhumiwa kuiba Sh 15,000

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Kalangalala iliyopo mjini Geita ameuawa kwa kupigwa mateke na ngumi akituhumiwa kuiba Sh 15,000 kwenye duka lililopo jirani na nyumba yao.

Geita. Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Kalangalala iliyopo mjini Geita ameuawa kwa kupigwa mateke na ngumi akituhumiwa kuiba Sh 15,000 kwenye duka lililopo jirani na nyumba yao.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe amesema tukio hilo limetokea Aprili 7,2021 wakati mtoto huyo akipatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa wa Geita.

Kamanda amesema mtoto huyo alishambuliwa na mwenye duka  Hamad Juma aliyetoroka baada ya tukio hilo na jeshi la polisi linamsaka.

“Mtoto huyu indaiwa alikuwa anaiba dukani na mtuhumiwa alimkamata na kumuadhibu sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha kifo chake”amesema Mwaibambe

Akizungumza na Mwannachi Digtal, bibi wa marehemu Grace Mathias amesema Aprili 7,2021 saa moja asubuhi akiwa amelala aliitwa na wanae wanaolala chumba cha nje na alipotoka alimkuta mjukuu wake akiwa amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake.


Amesema alimpeleka mjukuu wake hospitali na kupata matibabu ya awali lakini wakati akiendelea na matibabu alipoteza maisha .

“Mimi naomba Serikali ichunguze jambo hili huyu mtoto nimemlea tangu akiwa na miezi saba baada ya mama yake kufariki sasa ana miaka 13 sijawahi kusikia malalamiko popote kuwa ni mdokozi na wapo ndugu zake anakuwa nao wakati wote mimi naiachia Serikali”amesema Grace.

Lucas Pastory jirani wa familia amesema jamii inapaswa kufuata sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwakuwa matukio ya ukatili ynaazidi kuongezeka kila kukicha.