Mwanafunzi bora Udom azungumzia rushwa ya ngono

Mwanafunzi bora kwa mwaka 2023 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Nevi Nzowa.

Dodoma. Nevi Nzowa (23), mhitimu wa Shahada ya Hisabati na Takwimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), aliyeibuka mwanafunzi bora wa mwaka 2023, amesema baadhi ya wanafunzi vyuoni hutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono.

Nevi alitunukiwa shahada na tuzo ya mwanafunzi bora kwa mwaka 2023 na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda katika mahafali ya 14 ya Udom, yaliyofanyika juzi jijini hapa.

“Napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa mwanafunzi bora. Ninachoamini ni kwamba, kusoma kunaleta heshima, natamani nisome hadi kufikia uprofesa,” alisema.

Kuhusu madai ya rushwa ya ngono katika vyuo vikuu, Nevi alisema ingawa hajawahi kukutana na changamoto hiyo, kuna wakati wasichana hutengeneza mazingira ya uwepo wake.

Alisema mtu anakuwa mzembe darasani, hasomi, anapopata matokeo mabaya huanza kuhangaika.

“Wanafunzi wangesoma na kujitambua, wangeepuka habari za rushwa ya ngono vyuoni, aliyesoma huwa na mawazo, fikra na utendaji tofauti.”

Nevi, aliyepata ufaulu wa GPA 4.5, alisema alikuwa akitumia muda wa mapumziko kusoma na kujadiliana na wenzake.

“Bwenini pia nilikutana na watu wasioelewa, kuna wakati unaposoma wao hufungua muziki,” alisema.

Nevi, mtoto wa kike pekee katika familia ya watoto wanne ya Nzowa, alisema malengo yake ni kujiendeleza na masomo, akijiandaa kuomba udhamini ili kusoma shahada ya pili.

Akizungumzia hisabati, somo ambalo huwashinda wanafunzi wengi, alisema: “Kipendacho roho hula nyama mbichi, somo la Hisabati kwa kweli nalipenda na nawaambia wenzangu siyo somo gumu”.

Kwa upande wake, Flora Julius, mama mzazi wa Nevi alisema tangu akiwa mdogo binti yake alikuwa na ushirikiano na watoto wa kiume waliomsaidia katika masomo.

Alisema baada ya kujiunga Udom, katika mawasiliano ya simu usiku alikuwa akimwambia yupo kwenye majadiliano na wenzake wa kiume kwa kuwa hakuwa akipendezwa na mambo waliyokuwa wakiyafanya wenzake wa kike. “Nilikuwa namwambia angalia wasikudanganye, yeye aliniambia anajitambua hawezi kufanya ujinga akaacha kilichompeleka chuoni.

Nilimwamini kwa sababu pia anapenda kusali,” alisema.

“Wakati mwingine nikigombana na baba yake ananiambia ungesoma mama ungeheshimika. Ni mtoto anayejituma, akiwa nyumbani hataki nifanye kazi, huzifanya zote,” alisema.

Alisema katika mitihani ya kumaliza darasa la saba alipata wastani wa B, matokeo ya kidato cha nne alipata daraja la pili ponti 21 na kidato cha sita alipata daraja la kwanza pointi tisa.