Mwanafunzi Chuo Kikuu Ardhi aibuka mshindi shindano la DSE

Muktasari:

Soko la hisa  Dar es Salaam (DSE) kupitia shindano lake la uwekezaji kwa wanafunzi (DSE-SIC) leo Alhamisi Januari 21, 2021  limemtangaza mshindi kwa mwaka 2020.

Dar es Salaam. Soko la hisa  Dar es Salaam (DSE) kupitia shindano lake la uwekezaji kwa wanafunzi (DSE-SIC) leo Alhamisi Januari 21, 2021  limemtangaza mshindi kwa mwaka 2020.

Katika shindano hilo lililohitimishwa leo mwanafunzi wa mwaka wa nne Chuo kikuu cha Ardhi, Bakari Nassoro ameibuka mshindi kati ya watu 17,255 na kuzawadia Sh1 milioni.

Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Aston Ngaeje aliyepewa Sh500,000, watatu ni Pascal Projestus Sh300,000, na  wanne Magoma Bele Sh200,000 na watano Emmanuel Sai aliyepata Sh100,000.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimishwa kwa shindano hilo ambalo hudhaminiwa na benki ya Azania mkurugenzi mkuu wa DSE, Moremi Marwa amesema tangu kuanza kwa mashindano hayo mwaka 2014 wanafunzi zaidi ya 50,000 wameshiriki.

"Lengo la mashindano haya ni kuwapa fursa wanafunzi wa sekondari na elimu ya kuelewa masuala masoko ya mitaji na fedha na kwa kulielimisha kundi hilo tunawafikia wengi ambao wanafahamiana nao," amesema.