Mwanafunzi mbaroni akidaiwa kumjeruhi mwenzake na bisibisi
Muktasari:
- Chanzo cha tukio hilo inadaiwa kuwa, mtuhumiwa alimwomba mwenzake Amos Obiero amwongezee fedha kwa ajili ya kunyolea baada ya kukataliwa, alimvizia Amos akiwa njiani na kumjeruhi kwa bisibisi.
Musoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Sirari iliyopo wilayani Tarime, Denis Mwita kwa tuhuma za kumchoma bisibisi ya sikioni mwanafunzi mwenzake wa kidato cha tatu, Amos Obiero (17) na kumsababishia ulemavu wa sikio la kushoto.
Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa bisibisi hiyo iliingilia sikio la kushoto na kutoboa ngoma ya siku hadi kugusa sehemu ya uti wa mgongo kwenye kisogo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Oktoba Mosi, 2024, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mark Njera amesema chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa kumuomba majeruhi amwongeze fedha kwa ajili ya kunyolea, baada ya kukataliwa, mtuhumiwa huyo alimvizia majeruhi akiwa njiani kurudi nyumbani na kumjeruhi na bisibisi.
"Huyu Amos hata alipovamiwa na mwenzie hakuwa na wasiwasi kwani wao ni marafiki wa siku nyingi hata wazazi wao pia ni marafiki wakubwa tu, tumemkamata mtuhumiwa leo asubuhi na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika," amesema Kamanda Njera.
Kufuatia tukio hilo mwanafunzi huyo, amepoteza uwezo wa kusikia kwa upande wa sikio lake la kushoto baada ya ngoma ya sikio kutobolewa.
Akizungumza leo Oktoba Mosi, 2024, hospitalini hapo mwanafunzi huyo mkazi wa Kijiji cha Kanisani wilayani Tarime, amesema Septemba 29, 2024 jioni akiwa saluni ananyoa rafiki yake aitwaye Denis Mwita alifika saluni hapo na kumuomba amuongezee Sh100 ili anyoe, kwani alikuwa na Sh400 tu.
"Nilimwambia sina hiyo hela akaanza kunitania eti nanuka mdomo na mimi nikamtania ananuka jasho sikujua kama amekasirika nilipomaliza kunyoa nikaondoka akanifuata kwa nyuma, kisha kunipiga ngumi na kunichoma na kitu sikioni,” amesema.
Akieleza chanzo cha tukio hilo, mama wa mwanafunzi huyo, Eufracia Obiero amedai ni kutokana na deni la Sh350, 000 ambalo mwanaye anamdai mtuhumiwa huyo.
Amesema mwanaye alimpa mtuhumiwa huyo fedha hizo ili amuagizie kompyuta mpakato (laptop) kutoka Mwanza, lakini hakuileta wala kurejesha fedha.
Amesema kutokana na deni hilo, mwanaye aliamua kumshtaki mwenzie kituo cha Polisi Sirari, ambapo askari wa kituo hicho waliwaita wazazi wa pande zote kwa ajili ya hatua zaidi.
"Waliona hawa ni watoto ikabidi watushirikishe wazazi na tulipofika pale kwa vile hawa watoto ni marafiki wa siku nyingi sisi wazazi tuliamua kesi hiyo tutaimaliza wenyewe, ambapo wazazi wa Denis waliahidi kulipa pesa hizo.
"Nadhani ni Agosti, baada ya mwanangu kuona halipwi pesa zake wala kupewa alichoagiza na makubaliano ya wazazi hayatimizwi, ndipo alipoamua kwenda Polisi," amesema.
Baba wa mwanafunzi huyo, Paskali Obiero amesema siku ya tukio akiwa anaangalia mpira alipigiwa simu na mke wake ambaye pia hakuwepo nyumbani kwa muda huo, akimtaarifu juu ya kijana wao kujeruhiwa.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo alikwenda nyumbani na kumuwahisha kijana wake katika kituo cha afya binafsi kilichopo Sirari, ambapo hata hivyo aliambiwa hakina uwezo wa kumtibu na kutakiwa kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu zaidi na ya haraka.
"Ilikuwa saa 2 usiku ikabidi tupitie kituo cha Polisi kuchukua PF3 baada ya hapo tukaenda moja kwa moja Tarime ambapo baada ya kupokelewa walisema inabidi mgonjwa apewe rufaa kuja hospitali ya mkoa na tuliondoka usiku huohuo kuja hapa,” amesema.
Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk Lesso Mwinyimkuu amesema mgonjwa huyo alipokelea hospitalini hapo saa 7 usiku wa kuamkia jana.
"Baada ya kumpokea tulimfanyia uchunguzi ikiwa ni pamoja na kumfanyia vipimo vya CT – Scan, lakini bahati nzuri pamoja na kujeruhiwa vibaya, lakini bado alikuwa na uwezo wa kutembea na mikono yake pia ilikuwa inafanya kazi.
Amesema baada ya uchunguzi walibaini kuwa bisibisi hiyo imeingilia sikio la kushoto na kutoboa ngoma ya siku hadi kugusa sehemu ya uti wa mgongo kwenye kisogo.
"Alifika hapa akiwa bado ana bisibisi ambayo iliingia kama inchi saba hivi na tulifanikiwa kuitoa vizuri baada ya kumfanyia upasuaji na sasa anaendelea vizuri ingawa awali alivuja damu nyingi, lakini tulifanikiwa kuzuia damu isitoke zaidi na sasa anaendelea vizuri," amesema Dk Mwinyimkuu.
Amesema kutokana na majeraha aliyoyapata mwanafunzi huyo amepoteza uwezo wa kusikia kwa sikio lake la kushoto na ili lisikie tena atahitajika kufanyiwa upasuaji mara ya pili, ambapo upasuaji huo unaweza kufanyika baada ya kupona kabisa majeraha ya sasa.