Mwendo kasi waponza madereva 900 Shinyanga

Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi akionesha baadhi ya pikipiki zilizokamatwa katika msako na operesheni iliyofanyika mwezi mmoja uliopita. 

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewakamata madereva zaidi ya 900 kwa tuhuma za kukiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuendesha vyombo vyao kwa mwendo kasi kati ya 80 hadi 89.

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewakamata madereva zaidi ya 900 kwa tuhuma za kukiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuendesha vyombo vyao kwa mwendo kasi kati ya 80 hadi 89.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 26, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema madereva hao wamekamatwa katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya misako na operesheni kufanyika na kukamata madereva hao na pikipiki 1, 417.

Amesema katika operesheni hiyo pia wamekamata magari 944 kutokana na madereva kuendesha kwa mwendo hatarishi na kuwafikisha Mahakamani madereva 11 wa kampuni mbalimbali wanaoendesha mabasi ya abiria kwa mwendo kasi.

“Katika kuendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi la polisi tunaendelea  kutoa elimu ya kubaini viashiria vya uhalifu na wahalifu, pia kufanya misako na operesheni mbalimbali na kutoa elimu kwa madereva na waendesha pikipiki,”amesema Magomi

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limekamata mirungi bando 24, bangi kete 206 zikiwa nyumbani kwa mtu, vifaa vinavyotumika kupiga ramli chonganishi, mabati 19 na vipande vya chuma ambavyo ni alama za barabarani.

Magomi ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu pamoja na kuwafichuwa wanaofanya uhalifu, huku akiwataka madereva na waendesha pikipiki kutii na kuheshimu alama, michoro na sheria za barabarani.