Mwenge kukagua miradi 29 ya Sh6 bilioni Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere (kulia) akimkabidhi mwenge wa uhuru Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, ulipopokelewa mji mdogo wa Mirerani ambapo utatembelea miradi 29 ya sh6.6 bilioni. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Mwenge wa uhuru umeingia mkoani Manyara na unatarajia kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ambayo yatawekwa mawe ya msingi, kukaguliwa na kuzindua miradi 29 yenye thamani ya Sh6.6 bilioni.

Simanjiro. Mwenge wa uhuru umeingia mkoani Manyara na unatarajia kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ambayo yatawekwa mawe ya msingi, kukaguliwa na kuzindua miradi 29 yenye thamani ya Sh6.6 bilioni.

 Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere, leo ijumaa Juni 11, akiwa katika mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, ameupokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai, ambapo amesema utakimbizwa kwa kilomita 1,089.3.

Makongoro amesema mwenge huo utaweka mawe ya msingi ya miradi 10 yenye thamani ya sh3.7 bilioni na kuzindua miradi minne yenye thamani ya Sh342.3 milioni.

Amesema pia utafungua miradi mitatu yenye thamani ya Sh534.3 milioni na kukagua miradi 12 yenye thamani ya Sh2 bilioni.

"Mwenge wa uhuru utakimbizwa kwenye tano za Simanjiro, Kiteto, Babati, Hanang' na Mbulu, kisha tutaukabidhi kwa Mkoa wa Arusha Juni 16," amesema Makongoro.


Mwalimu wa mazingira wa shule ya Sekondari Mgutwa, Exaud Mafie amesema mradi wa mazingira uliozinduliwa na mwenge umegharimu Sh16.7 milioni.

Mafie amesema katika mradi huo, shule ya Mgutwa imechangia Sh16.7 milioni, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Sh1.6 milioni, Malihai Club Sh125,000 na Maivaro Ever Green Sh6 milioni.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Josephine Mwambashi amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tehama ni msingi wa Taifa endelevu itumie kwa usahihi na uwajibikaji’.