Mwenge kuwashwa Njombe, kuzimwa Kagera 2022

Miradi ya Sh15.3 bilioni yakataliwa na Mwenge wa Uhuru

Muktasari:

  • Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 zitafanyika mkoani Njombe na kuhitimishwa Kagera


Chato. Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 zitafanyika mkoani Njombe na kuzimwa Kagera

Akitoa taarifa ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Oktoba 14, 2021 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema mbio hizo zitahitimishwa mkoani Kagera.

"Tunawashukuru viongozi wa mikoa hiyo miwili kwa utayari wa sherehe hizo, naamini mmeona makubwa yaliyotendeka wakati wa uzinduzi na hitimisho wa mbio za mwaka huu. Hivyo jiandaeni vema," amesema Waziri Mhagama.

Mwaka huu Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika wilaya 150 ambapo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imeibuka kidedea kwa vigezo vya ubora wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wilaya zingine zilizoibuka na ushinda wa kikanda ni Nyamagana, Shinyanga, Muleba, Ruangwa na Kusini Unguja.

Wilaya hizo pamoja na mikoa ya Kusini Unguja na Geita zilizokuwa wenyeji wa sherehe za uzinduzi na hitimisho wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimepata zaidi ya vyeti, vikombe na fedha taslimu.