Mwenge: Miradi Sh30.3 bilioni kuonwa Kilimanjaro
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim kushoto, akipokea maelezo ya mradi wa maji Kirinjiko
Muktasari:
- Jumla ya miradi 45 yenye thamani Sh30.3 bilioni inatarajiwa kutembelewa na Mwenge wa uhuru katika halmashauri 7 za mkoa wa Kilimanjaro, ambapo miradi 17 itakaguliwa, 13 kitafunguliwa na kuzinduliwa na mingine 15 itawekwa mawe ya Msingi.
Same. Jumla ya miradi 45 yenye thamani Sh30.3 bilioni inatarajiwa kutembelewa na Mwenge wa uhuru katika halmashauri 7 za mkoa wa Kilimanjaro, ambapo miradi 17 itakaguliwa, 13 kitafunguliwa na kuzinduliwa na mingine 15 itawekwa mawe ya Msingi.
Hayo yamesemwa leo Juni 20 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu wakati akipokea Mwenge wa uhuru katika shule ya Msingi Chekereni, Kata ya Mabilioni, wilayani Same ukitokea Mkoa wa Tanga ambapo Kilimanjaro utakimbizwa kilomita 918.
Babu amesema miradi hiyo imegusa sekta zote ambazo ni Elimu miradi 9, Afya miradi 9, Maji miradi 7, utunzaji mazingira miradi 7, Barabara na madaraja miradi 6, Vijana miradi 5 na miradi mengineyo miwili," amesema RC Babu na kuongeza kuwa;
"Mwenge wa uhuru ukiwa katika mkoa wa Kilimanjaro utapata fursa ya kuona na kutembelea juhudi mbalimbali zinazofanywa na vikundi vya vijana, walemavu na wanawake katika kuzalisha mali ili waweze kujiendeleza kiuchumi, utazinduka klabu za kupambana na rushwa na kutembelea maonesho mbalimbali ya shughuli za elimu.”
Aidha Babu amesema, katika Wilaya ya Same ambako Mwenge huo umepokekewa, utakimbizwa Kilometa 99.6 ambapo utatembelea miradi 7 yenye thamani ya Sh3.6 bilioni.
Miradi hiyo n pamoja na ufunguzi wa barabara ya Hedaru -Vunta-Myamba, uzinduzi wa madarasa mawili katika shule ya Sekondari Chauka, kuweka jiwe la msingi zahanati ya Saweni, kugawa vyandarua pamoja na uzinduzi wa mradi wa maji Mwembe.