Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi ya Sh9 bilioni Kigamboni

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa  Abdalllah Shaib akimwaga maji kwenye barabarara ya Tungi Mjimwema ili kuangalia kama imekidhi  viwango.

Muktasari:

  • Mwenge wa Uhuru unatarajia kukagua na kuzindua miradi sita iliyogharimu Sh 9 bilioni  katika Wilaya ya Kigamboni, ikiwa ni mwendelezo wa mbio za Mwenge Kitaifa zilizozinduliwa Aprili Mosi mwaka huu.

Dar es  Salaam. Jumla ya miradi sita yenye thamani ya Sh 9 bilioni inatarajiwa kukaguliwa  na  kuzinduliwa kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru utakaokimbizwa katika Wilaya ya Kigamboni.

Mwenge huo unakimbizwa leo Alhamisi Mei 25, 2023 jatika Wilaya hiyo ukitokea Temeke ambapo ulikagua na kuzindua miradi sita iliyogharimu Sh 13 bilioni.

Jana Mwenge wa Uhuru uliwasili jikini Dar es Salaam ukitokea Mafia mkoani Pwani na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila.

Hata hivyo akipokea Mwenge huo Chalamila alisema, utakimbizwa katika wilaya zote za Dar es Salaam na kuzindua miradi 32 itakayo gharimu Sh 96 bilioni.

Akizungumza wakati akipokea mwenge huo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo amesema katika miradi hiyo, ipo iliyokamilika na mingine iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

"Miradi hii ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya afya, na miradi ya maji ni miradi inayotekelezwa na fedha za ndani, zipo fedha zinazotoka Serikali Kuu na nyingine kwenye halmashauri," amesema Bullembo.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Abdalllah Shaib amesisitiza wananchi kuzingatia kaulimbiu ya mbio za Mwenge kwa mwaka 2023 inayosisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji, kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa taifa.

Pia kiongozi huyo aliitaka jamii kupiga vita rushwa na  kuhimiza lishe bora, kupambana na ugonjwa malaria pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Aprili Mosi mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa katika Viwanja vya Nangwanda Sijaona ambapo utakimbizwa nchi nzima kukagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.