Mwenyekiti Halmashauri Mufindi awaonya watendaji waliopewa pikipiki

Miongoni mwa pikipiki zilizotolewa na Halmashauri ya Mufindi mkoani Iringa kwa ajili ya maofisa watendaji kata kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi za kila siku. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

  • Akizungumzia na Mwananchi leo Alhamisi Januari 26, 2023 Mgina amesema  kuwa halmashauri hiyo ilitenga bajeti ya kununua pikipiki 27  yenye thamani  Sh81 milioni ili kuwarahisishia utendaji wa kata kufanya kazi zao kwa urahisi katika ufuatilijia wa  miradi ya maendeleo  kwenye maeneo yao kwa wakati.

Mufindi. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Festo Mgina wamewataka watendaji wa kata zote za halmashauri hiyo kuhakikisha wanatumia  pikipiki walizogaiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na watakaotumia kinyume watanyang'anywa pikipiki hiyo.

Akizungumzia na Mwananchi leo Alhamisi Januari 26, 2023 Mgina amesema  kuwa halmashauri hiyo ilitenga bajeti ya kununua pikipiki 27  yenye thamani  Sh81 milioni ili kuwarahisishia utendaji wa kata kufanya kazi zao kwa urahisi katika ufuatilijia wa  miradi ya maendeleo  kwenye maeneo yao kwa wakati.

Aidha amesema kuwa pikipiki hizo ambazo zimegaiwa ni mali ya halmashauri  hivyo mtendaji yoyote akipatika anafanya biashara ya bodaboda tofauti na matumizi ambayo yamekusudiwa hawatasita kuichukua  na kupeleka sehemu nyingine kwa watendaji wa vijiji kwa sababu hawana usafiri huo.

"Hizi ni mali za Serikali hivyo wakizitumia vibaya hatutasita kuzichukua na kuwapa watu wengine kama watendaji wa vijiji ambao wanahitaji  kwa kufuata kanuni zinazolinda mali za halmashauri  kama ambavyo tunafanya kwa wakuu wa idara,"  Amesema Mgina.

Pia Mwenyekiti huyo amesema kuwa  halmashauri hiyo umejipanga kununua pikipiki zingine 221  kwa ajili ya kuwagawia watendaji wa vijiji ili waweze kuteketeza majukumu yao kuwa urahisi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mninga,  Ada Lwangiri  ameshukuru halmashauri hiyo kwa kuwagawia pikipiki hizo jambo ambalo litawasidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Tunaishuru halmashauri yetu kwa kutugawia  pikipiki 27 kulinga na idadi ya kata  kwa sababu zitatisaidia kurahisisha utendaji wetu hasa katika ufuatijia wa miradi ya maendeleo ambayo ipo kwenye kata na vijiji katika maeneo yetu pamoja na ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo," amesema Lwingiri.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mdaburo Donald Mgaya amesema kuwa halmashauri imewasaidia kuwawezesha nyenzo muhimu ya usafiri wa pikipiki kwa sababu awali walikuwa wanapata changamoto kubwa ya umbali wa maeneo katika ufuatijia wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa.