Mwenyekiti wa Kijiji kortin akidaiwa kuteketeza matrekta

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kijiji cha Engong'ongare mkoani Manyara, Baraka Koisenge (53) na wenzake 10 wamefikishwa katika mahakama ya wilaya kwa makosa mawili ya kuteketeza matrekta kwa kuweka chumvi injini na wizi.

Kiteto. Mwenyekiti wa Kijiji cha Engong'ongare mkoani Manyara, Baraka Koisenge (53) amefikishwa katika mahakama ya wilaya kwa makosa mawili yakiwemo kuteketeza matrekta kwa kuweka chumvi injini na wizi.

Katika kesi hiyo namba 3 ya 2023, mwenyekiti huyo pamoja na wenzake wanatuhumiwa kuchoma vibanda vya wakulima kuteketeza  eneo la Muturo kijiji cha Engong'ongare, kuteketeza matrekta matatu ya wakulima kwa kuweka chumvi kwenye injini na kukatakata matairi.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Joseph James akiwa mahakamani hapo leo Jan 13, 2023 amemsomea mashtaka Mwenyekiti huyo Baraka Kwaisenge mashtaka mawili, ambayo ni kuteketeza matrekta, kuiba vifaa pamoja na kuchoma vibanda.


Amesema mnamo Desemba 30, 2022 mtuhumiwa akiwa na wenzake 10 waliteketeza matrekta kwa kuweka chumvi kwenye injini na kosa lingine ni kuiba vifaa vya matrekta hayo sambamba na kuchoma vibanda vya wakulima wa Kijiji hicho.

Mshtakiwa huyo alikana mashitaka hayo mahakamani hapo, ambapo mwendesha mashitaka wa Serikali Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Joseph James alimweleza hakimu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba hakimu, Boniphas Lihamwike kutaja tarehe nyingine kwa ajili ya hoja za awali.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Feb 9, 2023 ambapo hakimu Boniphas Lihamwike alionya kuwa kama upelelezi huo hautakamilika ataondoa kesi hiyo hapo mahakamani

Amesema dhamana ya mtuhumiwa huyo iko wazi na masharti yake ni watu wawili  wakiwa na Sh2 milioni kila mmoja.