Mwili wa mwanzilishi wa Precision Air wawasili kijijini kwao
Mwili wa Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya shirika la ndege la Precision Air, Michael Ngaleku Shirima ukiwasili jioni hii nyumbani kwake katika Kijiji cha Nayeme, Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Rombo. Mwili wa Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Shirika la Ndege la Precision Air, Michael Ngaleku Shirima umewasili katika Kijiji cha Nayeme, Tarakea, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Mzee Ngaleku alifariki usiku wa Juni 9, mwaka huu katika Hospitali ya Aghakan, Dar es salama alikokuwa amelezwa Juni 8 atazikwa kesho Juni 15 kijijini hapo katika makaburi ya familia.
Mwili huo umewasili kijijini kwake jioni hii ulipokelewa na mamia ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara mashuhuri wa Mkoa wa Kilimanjaro, watawa wa kanisa Katoliki ambao wanahudumu katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Ngaleku kituo ambacho alikijenga Mzee Ngaleku pamoja na viongozi wa chama na serikali wa mkoa huo.
Hata hivyo mwili wa mfanyabiashara huyo nguli wa anga, umesindikizwa na viongozi mbalimbali wa serikali kutokea Jijini Arusha akiwemo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, baadhi ya wabunge wa Bunge la Tanzania, wafanyabiashara mashuhuri nje na ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na viongozi wengine waliokuwepo katika msafara huo.