Mwinyi: Tulidhibiti vyama kuungana

Mwinyi: Tulidhibiti vyama kuungana

Muktasari:

  • Asema Nyerere alitaka kuwepo na mgombea binafsi lakini walio wengi ndani ya chama walisema hiyo itadhoofisha CCM.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameeleza jinsi mfumo wa vyama vingi ulivyoingia nchini na kuleta tishio la kusambaratika kwa CCM akisema ilibidi wadhibiti vyama vya upinzani kuungana na suala la mgombea binafsi.

Mwinyi maarufu kwa jina la Mzee Rukhsa ameyaeleza hayo katika kitabu chake cha ‘Mzee Rukhsa: Safari ya maisha yangu’ kilichozinduliwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Mzee Mwinyi imekuja ikiwa imepita miaka 28 ya mfumo wa vyama vingi vianze nchini huku vikiwa vinalalamikia masuala mbalimbali likiwemo kuzuiwa kuungana.

Katika harakati zake, upinzani nchini umeishia tu kushirikiana katika baadhi ya maeneo kama ilivyofanyika kwa kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioanzishwa mwaka 2014 wakati wa Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kushirikiana kwa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na NLD karika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika kitabu hicho, Mwinyi ameeleza jinsi mfumo wa vyama vingi ulivyozua mjadala mkali katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika katika ukumbi wa Diamon Jubilee jijini Dar es Salaam, Februari 21, 1992.

“Tulijitahidi kufanya iwe vigumu kwa vyama kuungana, tukasema wakitaka kuungana lazima wajifute kwanza na kisha kuanza kujisajili upya,” anasema Mwinyi katika kitabu hicho.

Mbali na kuungana kwa vyama, Mwinyi anaeleza kuwa pia ulitokea mvutano kuhusu hoja ya mgombea binafsi.

“Tulishindana kwenye jambo moja tu – la wagombea binafsi Mwalimu Julius Nyerere yeye alitaka wawepo, lakini wengi kwenye chama na Serikali walihofu, kwa haki kabisa, kuwa hiyo itakuja kuidhoofisha CCM, pale wasipopita kwenye mchujo wakiamua kusimama kama wagombea binafsi,” anaeleza Mwinyi.

Hata hivyo, akifafanua zaidi katika kitabu hicho, Mwinyi anasema hatua hizo mbili, kudhibiti kuungana kwa vyama na kuzuia mgombea binafsi, hazikulenga kuipendelea CCM bali kuimarisha mfumo wa vyama vingi.

“Ukiendeleza wagombea binafsi na vyama kuungana kirahisi unaishia kudhoofisha vyama kama taasisi muhimu na mhimili wa siasa za upinzani.

“Badala ya kujiimarisha na kujiandaa kuwa Serikali mbadala, vitakuwa vinatafuta tu mbinu za kushinda uchaguzi.

“Hatimaye kutakuwa hakuna vyama madhubuti bali mashirikiano tu kwa ajili ya kutafuta ushindi kwenye uchaguzi. Katika mazingira hayo ya vyama dhaifu, hata kusimamia nidhamu ndani ya vyama itakuwa taabu,” anasema.


Sakata la mgombea binafsi

Harakati za kupigania mgombea binafsi lilianza mwaka 1993 baada ya Mchungaji Christopher Mtikila kufungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira aliyempa ushindi Mchungaji Mtikila.

Hata hivyo, mwaka 1994 Serikali iliwasilisha bungeni mapendekezo ya kubadilisha Ibara ya 34 ya Katiba na kuzuia wagombea binafsi. Mwaka 2005, Mtikila alifungua tena kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo.

Kesi hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Amir Manento, pia walikubaliana na hoja za Mchungaji Mtikila. Hata hivyo, mwaka 2010, Serikali ilikata rufaa kupinga uamuzi huo.

Jaji mkuu wa wakati huo, Augustino Ramadhan aliongoza jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa kusikiliza kesi hiyo, kisha wakatoa hukumu ambayo ilikosolewa vikali, kuwa si jukumu la Mahakama kujielekeza kwenye masuala ya kisiasa.

Hata hivyo, Mchungaji Mtikila ambaye sasa ni marehemu, alifungua kesi nyingine katika Mahakama ya Afrika jijini Arusha na alishinda kesi hiyo mwaka 2013 na Mahakama hiyo iliitaka Serikali kutekeleza hukumu hiyo lakini hadi hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.


Moto wa vyama vingi

Akifafanua suala mfumo wa vyama vingi kwa ujumla, Mzee Rukhsa anasema katika vuguvugu la mfumo huo lilitokana na shinikizo la kimataifa lililoanza miaka 1980 baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti (USSR) baada ya aliyekuwa Rais wa Urusi, Mikhail Gorbachev kuingia madarakani na kukomesha vita baridi.

Ametaja pia mabadiliko yaliyotokea nchi za Poland, Yugoslavia na Ujerumani baada ya ukuta uliotenganisha Ujerumani Masharini na Magharibi kuvunjwa kuwa kichocheo cha mfumo huo.

Nchini Tanzania, amesema majadiliano ya kuruhusu mfumo wa vyama vingi yalianza tangu mwaka 1989.

“Kwenye kikao chake kilichofanyika Dodoma, Oktoba 11-14, 1989, Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), pamoja na mambo mengine, tulijadili kidogo vuguvugu la mageuzi lililokuwa limeenea katika baadhi ya nchi za kijamaa, hususani Urusi na Ulaya ya Mashariki.”

Ametaja baadhi ya mikutano iliyojadili mageuzi kuwa pamoja na mkutano wa NEC wa Februari 1990 ambapo Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alitoa mada ya mabadiliko yaliyokuwa yakitokea barani Ulaya na athari zake kwa Afrika.

Mwinyi anasema baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu uenyekiti wa CCM mwaka 1990 majukumu yote yakamwangukia yeye, alishauriwa kuunda Tume kwa ajili ya kutafuta maoni ya uwepo wa vyama vingi.

“Februari 1991 niliunda Tume ya Rais kuhusu mfumo wa wa kisiasa nchini, iwapo tuendelee na mfumo wa chama kimoja au tuingie mfumo wa vyama vingi,” ameandika Mwinyi.

Ameandika wakati huo pia kulikuwa na mavuguvugu ya watu waliotaka mfumo huo akilitaja kundi la wasomi lililoitwa National Committee for Constitutional Reform lililokuja kuzaa chama cha NCCR- Mageuzi.

“Jambo lililonishangaza ni pale ripoti ilipoonyesha kuwa, takribani asilimia 20 tu ya Watanzania ndio walitaka turejee kwenye mfumo wa vyama vingi.”

Hata hivyo, alisema baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo ilionekana wananchi wengi waliotaka mfumo wa chama kimoja pia walitaka mabadiliko katika mambo mengi.

“Tume ya Jaji Nyalali ikashauri ni vema tuingie tu kwenye mfumo wa vyama vingi,” imesema sehemu ya kitabu hicho.

Wakati mfumo huo uko mbionikuanza, Mwinyi anasema vurugu za kisiasa zilianza huku akiwataja baadhi ya waanzilishi wa mageuzi aliosema walikuwa wasumbufu.

“Miongoni mwa waliotusumbua walikuwa pamoja na Chief Abdallah Fundikira, Oscar Kambona, Seif Sharif Hamad, James Mapalala (wote marehemu) na Mabere marando,” alisema.

Hata hivyo, alisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema (sasa Mwenyekiti wa TLP) aliwadhibiti.

“Lakini ikabidi na CCM nayo izinduke na kuanza kutafuta wanachama wengi zaidi kabla ya vyama vingi havijaruhusiwa,” anasema.

“Baada ya kuisoma ripoti nikamuita Ikulu Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru (comrade), nikamsimulia yaliyokuwepo katika ripoti, Comrade akajaribu sana kunishawishi kuwa turuhusu mfumo wa vyama vingi, ingawa naye alikiri kuwa itakuwa kazi kubwa kuwashawishi wapinzani wa mfumo wa vyama vingi, hasa kwa kuzingatia matokeo ya Tume ya Nyalali.