Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwongozo mpya kusaidia waishio maeneo ya migodi wazinduliwa

Baadhi ya viongozi wa dini na wawakilishi wa mashirika mbalimbali wakionesha mwongozo mpya wa kusaidia jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini kudai haki na uwajibikaji, baada ya uzinduzi wake jijini Arusha.

Muktasari:

  • Mwongozo huo mpya sasa utakwenda kuwasaidia wananchi wanao athiriwa na migodi kupata haki, fidia stahiki na uwajibikaji kutoka kwa kampuni za uchimbaji.

Arusha. Kutokana na changamoto zinazoendelea kuwakabilia wananchi wanaoishi maeneo ya uchimbaji madini, wadau wa maendeleo, mashirika ya dini na watetezi wa haki za binadamu kutoka Afrika Mashariki na Ukanda wa Maziwa Makuu wamezindua mwongozo maalumu utakaosaidia wananchi hao kupata haki na fidia stahiki.

Mwongozo huo uliozinduliwa jana Jumatatu Juni 8, 2026 jijini Arusha, unalenga kukabiliana na vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia wananchi wengi kupata suluhu, fidia na haki wanapodhuriwa na shughuli za uchimbaji wa rasilimali.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Meneja Programu wa Ushirika wa Mabaraza ya Kikristo na Makanisa katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika (FECCLAHA), Monica Njoroge, amesema umeandaliwa baada ya kubainika kuwa wananchi wengi wanaoishi karibu na migodi hukabiliwa na changamoto zinazofanana za ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amesema changamoto hizo ni pamoja na kupoteza ardhi, kuhamishwa kutoka maeneo yao bila fidia ya haki, mazingira yasiyo salama ya kazi na athari za kimazingira zinazotokana na shughuli za uchimbaji madini.

Baadhi ya viongozi wa dini na wawakilishi wa mashirika mbalimbali wakionesha mwongozo mpya wa kusaidia jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini kudai haki na uwajibikaji, baada ya uzinduzi wake jijini Arusha.

“Tumeona jamii zikibeba mzigo mkubwa wa athari za uchimbaji madini huku zikiwa na sauti ndogo katika kutafuta haki. Ndiyo maana tumeandaa mwongozo huu ili viongozi wa dini na mashirika mengine waweze kusimama pamoja na jamii hizo na kuzisaidia kutetea haki zao,” amesema Njoroge.

Ameongeza kuwa mwongozo huo unatarajiwa kusaidia jamii zilizoathiriwa kupata haki zao kwa kuweka mifumo bora ya kushughulikia malalamiko, kufuatilia madai ya fidia na kuongeza uwajibikaji wa kampuni zinazohusika.

Kwa mujibu wa Njoroge, FECCLAHA itaanza kwa kuwajengea uwezo viongozi wa dini katika nchi 10 za Afrika ili waweze kuelimisha wananchi kuhusu haki zao, kufuatilia malalamiko yanayohusiana na migodi na kushinikiza uwajibikaji wa kampuni za uchimbaji.

“Baadhi ya malalamiko yanayojirudia katika maeneo mengi ya uchimbaji madini ni ukiukwaji wa haki za ardhi, uhamishaji wa wananchi bila fidia ya kutosha, ukosefu wa usalama kwa wafanyakazi, hususan wanawake, pamoja na uchafuzi wa mazingira,” amesema.

Uzinduzi wa mwongozo huo umefanyika katika Jukwaa la Afrika Mashariki la Biashara, Haki za Binadamu na Mazingira, lililowakutanisha viongozi wa dini, mashirika ya kiraia, wataalamu wa haki za binadamu na wadau wa sekta ya madini kutoka nchi za Afrika Mashariki na Ukanda wa Maziwa Makuu.

Kwa upande wake, Ofisa Programu wa Shirika la Swedwatch la Sweden, Benjamin Claeson amesema tafiti za shirika hilo zimeonyesha kuwa jamii nyingi katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika zinakabiliwa na changamoto zinazofanana katika kutafuta haki baada ya kuathiriwa na shughuli za biashara na uchimbaji wa rasilimali.

“Mara nyingi wananchi hukosa njia madhubuti za kupata suluhu, fidia au majibu ya kuridhisha kutoka kwa kampuni zinazohusika. Hiki ni kikwazo cha kimfumo kinachohitaji suluhisho la kimfumo,” amesema Claeson.

Baadhi ya viongozi wa dini na wawakilishi wa mashirika mbalimbali wakionesha mwongozo mpya wa kusaidia jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini kudai haki na uwajibikaji, baada ya uzinduzi wake jijini Arusha.

Amesema mwongozo huo ni nyenzo muhimu kwa jamii na viongozi wa dini kwa kuwawezesha kushirikiana moja kwa moja na kampuni za uchimbaji madini na kutetea upatikanaji wa haki kwa waathirika.

Aidha, amesema mwongozo huo utatumika kuhamasisha kampuni zinazonunua malighafi katika nchi za Kaskazini mwa Dunia pamoja na wawekezaji wa kimataifa kutumia ushawishi wao kuhakikisha kampuni za uchimbaji zinazingatia haki na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya shughuli zao.

Naye Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Askofu Nelson Magori, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi wa Dini kuhusu Maadili na Uchumi, amesema haki za binadamu haziwezi kutenganishwa na maadili ya kiimani na utu wa binadamu.

“Huwezi kutenganisha haki za binadamu na mafundisho ya Mungu. Biashara njema ni ile inayojengwa katika misingi ya haki, uaminifu na heshima kwa utu wa kila mtu. Tunahitaji kuona uwekezaji unaozingatia haki za wananchi badala ya kuwa chanzo cha malalamiko na migogoro,” amesema Askofu Magori.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini watatumia mwongozo huo kushirikiana na wananchi kuwaelimisha kuhusu haki zao na kuhakikisha jamii zinashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi inayogusa maisha yao.