Mzee matatani kwa kujenga kaburi njiani

Muktasari:

  • John Nanyaro, mkazi wa Kijiji cha King’ori wilayani Arumeru ameingia katika mgogoro na wananchi baada ya kufunga barabara kwa kujenga kaburi akidai eneo hilo ni lake.

  


Arusha. John Nanyaro, mkazi wa Kijiji cha King’ori wilayani Arumeru ameingia katika mgogoro na wananchi baada ya kufunga barabara kwa kujenga kaburi akidai eneo hilo ni lake.

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, wakiwapo ndugu wa mlalamikiwa, wamesema barabara aliyofunga Nanyaro imekuwa ikitumiwa tangu mwaka 1991.

Mwenyekiti wa kamati ya mawasiliano wa kijiji hicho, Joel Nanyaro alisema wanapinga uamuzi ya ndugu yake, John kufunga barabara hiyo.

“Huyu ni ndugu yangu, anachokifanya ni kuvunja sheria na kutaka kupora ardhi hiyo ambayo yeye mwenyewe aliuza eneo hilo kwa marehemu Wilfred Urio,” alisema.

Mtoto wa marehemu Wilfred, Amani Urio alisema ameshangazwa na Mzee Nanyaro kumfungia barabara ya kwenda kwake na kujenga kaburi bandia usiku na sasa amekuwa akimtisha kuwa atampoteza.

Urio alisema aliamua kulifikisha suala hili katika Mahakama ya Mwanzo King’ori ambako hakimu alitoa hukumu kuwa kesi hiyo ipelekwe baraza la ardhi Novemba 5.

“Nimeshangazwa na uamuzi wa hakimu ambao nadhani una shinikizo la ninaowalalamikia kufunga barabara, kwani viongozi wote wa kijiji walitoa ushahidi kuthibitisha Mzee John kuvamia barabara,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha King’ori, Elipokea Nanyaro alisema yeye na viongozi wenzake wanatambua Mzee John amevamia eneo la barabara.

“Tulitoa ushahidi lile lilikuwa eneo la barabara tangu mwaka 1991 na lilitolewa kwa kufuata taratibu zote,” alisema.

Mzee wa ukoo wa Nanyaro, Cleopa Nanyaro pia alisema suala hilo lilishafikishwa katika kikao cha familia na Mzee John alitakiwa kurejesha ardhi anayoing’ang’ania.

Mzee John Nanyaro mwenyewe alisema eneo la barabara ni mali yake na amejenga kaburi la kijana wake.

“Mimi sijavamia eneo, hapa ni mali yangu hakuna barabara,” alisema Mzee John.

Hata hivyo, Hakimu wa Mahakama ya mwanzo King’ori, Prince Gedion alisema “kuna maneno mengi nimesikia, hata katibu tarafa alikuja ofisini kwangu kufuatilia jambo hili ambalo nimelipeleka baraza la ardhi kwani ni mgogoro wa ardhi.”