Mzee Mwinyi amsifu Rais Samia akisema ameanza vizuri

Mzee Mwinyi amsifu Rais Samia akisema ameanza vizuri

Muktasari:

  • Rais mstaafu Mwinyi alifika nyumbani kwa Rais Samia kumjulia hali na kumhakikishia kuwa yeye na wazee wenzake wako tayari kushirikiana naye.

Dar es Salaam. Rais wa  Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Dk Ali Hassan Mwinyi ambaye amempongeza kwa kuanza vizuri majukumu yake ya kuongoza nchi.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  leo Aprili 12, 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema kuwa Rais Mstaafu Mwinyi alifika nyumbani kwa Rais Samia kumjulia hali na kumhakikishia kuwa yeye na Wazee wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano wao.


“Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more (rudia tena). Ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha, kila raia unayemsikia anasema Mama ameanza vizuri,” amesema Rais mstaafu Mwinyi.


Ameendelea kusema kuwa Rais aliyekuwepo awali alikuwa mzuri mzoefu wa mambo ya Serikali.


“Sasa kaacha mambo haya ghafla kamuachia mwenzie, sasa Mama naye mwanadamu atakuwa na yake na vile vile kuna mambo ambayo yameanzwa na mtu mwingine ambayo watu wanayataka wanayapenda, wanamshikilia Mama tunayataka haya tunayataka!!, tulieni tutayatekeleza haya. Sasa hilo linafurahisha” amesema.


Aidha Msingwa amesema, Mwinyi amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa kuacha balaa, ugomvi na fitina badala yake wawe na umoja, mshikamano na kufanya juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.