Mzumbe kuhamasisha jamii kuthamini bima ya afya

Muktasari:

  • Jamii inayozunguka chuoni Kikuu Mzumbe imeanza kuhahamasishwa juu ya kupata bima ya afya kupitia mradi wake wa HEET.

Morogoro. Chuo Kikuu Mzumbe kupitia kitivo cha sayansi ya jamii kimeanza utaratibu wa kuhamasisha jamii inayozunguka chuoni hapo kuwa na bima ya afya kwani afya ni mtaji muhimu.

 Mhadhili wa kitivo Cha Sayansi ya Jamii Mzumbe, Dk Lihoya Chamwali amesema hayo Novemba 8, 2023 wakati wa mkutano wa ukataji wa Bima ya Afya na mchango wake katika kutatua changamoto zilizopo kwa wakazi wa Tarafa ya Mzumbe ulioandaliwa na Chuo Kikuu hicho kwa ufadhili wa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi kiuchumi (HEET Project) uliofanyika chuoni hapo.

Dk Chamwali amesena licha ya Serikali kuweka utaratibu wa bima ya afya lakini umiliki wa bima za afya kwa wananchi bado umekuwa mdogo.

Amesema mpaka mwaka 2021 asilimia 31 ya watu walikuwa wakimiliki bima za afya ambapo serikali inaendelea kusisitiza kila mwananchi lazima awe na bima ya afya kwa wote ili kusaidia katika upatikanaji wa mtaji ambao ni afya.

Aidha alisisitiza jamii kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya kwa kukata bima za afya kwani ni mtaji zaidi ya kuwekeza kwenye elimu na kuwekeza kwenye fedha kama ilivyosisitizwa zamani.

Dk Chamwali ambaye ni mfuatiliaji na mtathmini wa Mradi huo wa HEET, amesema ni vyema kila mwananchi akamiliki bima ya afya ili kujikinga pale anapopatwa na magonjwa kwani maradhi hayapigi hodi bali huja yenyewe.

“Nakumbuka zamani tuliambiwa tuwekeze kwenye elimu kwa watoto na fedha lakini siku hizi tunaambiwa afya na yenyewe ni mtaji, kwa sababu usipokuwa na afya hauwezi kufanya kazi na kupata fedha, nisingekuwa na afya nisingeweza kuja kazini,”amesema.

Mratibu, mtafiti na mbunifu katika mradi wa HEET Dk Christina Shitima ameeleza kuwa Mradi wa HEET unawezesha kupeleka mrejesho kwenye jamii ili kuboresha baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye tafiti zilizofanywa chini ya mradi huo.

Amesema umiliki wa bima ya afya unapaswa kwenda sambamba na kufika kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali kupatiwa matibabu badala ya kubaki na mitazamo hasi ya kupata dawa bila kupima.

Mmoja wa watafiti kutoka kitivo hicho cha sayansi ya jamii idara ya uchumi chuoni Mzumbe Felister Tibamanya ameshauri Serikali kupunguza gharama za upatikanaji wa Bima ya afya sambamba na miundombinu ya afya kuboreshwa ili kuchochea matumizi ya Bima miongoni mwa wanakaya.

Tibamanya amesema katika tafiti waliyofanya walipendekeza kutolewe elimu ya kutosha itakayochochea watu kujiunga na bima ya afya ikiwa ni pamoja na kuwaongezea vipato katika shughuli zao wanazofanya ili waweze kumudu gharama zilizopo kama hazitapunguzwa.

Aidha amesema Serikali iendelee kuwekeza kwenye afya kifedha kwa kutoa ruzuku za huduma za afya sambamba na kuboresha, kuanzisha ujenzi wa vituo vya afya karibu na makazi ya watu na kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya hasa vijijini. 

Amesema utafiti wa jumla umeonesha kuwa asilimia 26.2 ya wanakaya wanatumia bima ya afya kati ya wananchi 60 milioni waliopo nchini

Pia amesema utafiti huo umeonesha kuishi kijijini na umbali kutoka kituo cha afya vinapunguza matumizi ya huduma za afya sambamba na matumizi ya bima ni matokeo chanya katika matumizi ya huduma za afya.

Mkazii wa kijiji cha Changalawe Tarafa ya Mzumbe Paulo Mloka ameiomba Serikali kupunguza gharama ya upatikanaji wa bima ya afya hasa NHIF ili kusaidia hata wanavijiji kuipata ambao mpaka sasa wanadhani kuwa bima ya afya ni mtaji biashara ya mtu mmoja au taasisi moja kwa manufaa ya watu wachache.

Mradi wa HEET ni mradi uliopo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia unaendeshwa na Chuo kikuu hicho ukishirikisha wakazi kutoka vijiji vya Changalawe, Kipera, Mlali, Sangasanga Kiyenze na Mongwe vilivyopo tarafa ya Mzumbe Wilayani Mvomero mkoani hapa.